Wednesday, May 14, 2014

TAMWA wawalaani Boko Haram

ad300
Advertisement
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), mashirika na wanaharakati wanaotetea  haki za wanawake nchini wameungana kuiadhimisha siku ya familia duniani, kulaani kitendo cha kuwateka nyara wasichana takriban 200 kilichofanywa na waasi wa kikundi cha Boko Haram nchini Nigeria.

Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari, wawakilishi kutoka Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP), Jukwaa la Katiba (JUKATA) na  Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) walisema serikali ya Nigeria inapaswa kuongeza juhudi za kuwaokoa wasichana wale.

Walisema leo ni siku ya familia duniani, siku iliyoteuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kutambua wajibu wa kila mwanafamilia na serikali kuwajibika kuleta ustawi wa familia katika eneo husika kwa kuzingatia utu na haki za binadamu.

Kaimu Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi alisema siku hii ambayo kila mwanafamilia duniani anatakiwa awe na furaha hali itakuwa tofauti kwa familia zilizopoteza wapendwa wao wanaoshikiliwa na Boko Haram magharibi mwa bara la Afrika.

"Inasikitisha mno kuona siku ambayo mwenzako anafurahi wewe unakuwa unahuzuni. Ninaamini siku hii ni mbaya sana kwa familia zile kuliko siku yoyote tangu kupotea kwa wapendwa wao. Hivyo tunafanya hivi kuwaonesha tuko pamoja," alisema Lilian.

Naye Gladnes Munuo ambaye ni mjumbe wa kituo cha usuluhisho TAMWA, alisema wamebaini rasilimali ndio chanzo kikuu cha kuwepo kwa vikundi vibaya kama vya waasi, ambapo kukosekana kwa usawa kwenye mgawanyo ndio huleta hatari kama iliyotokea Nigeria.

Aidha kwa umoja wao walisema wanaamini kuwa mshikamano ndio njia pekee ya kuleta mafanikio kwenye mambo mengi hivyo wanaungana na dunia nzima kukemea vitendo vya unyanyasaji kama uliofanywa na Boko Haram.

Walisema serikali zote duniani zitambue kuwa wanawake na watoto ndio makundi ambayo yanapata shida kwenye hali mbalimbali ikiwemo kutumiwa kama chombo cha kutafutia haki, hivyo ulinzi zaidi unatakiwa kwenye makundi haya .

Pia walisema wameomba ruhusa kwa jeshi la Polisi  ili wafanye maandamano ya amani kuanzia katikati ya jiji la Dar es Salaam mpaka ubalozi wa Nigeria nchini ili kuonesha msimamo wao kuhusu kitendo kile kiovu.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: