Advertisement |
Mradi huo wa miaka mitano ulioanza 2008, unasimamiwa na Kampuni ya Belgium Technical Corporation (BTC) na umehusisha ujenzi wa visima vya kisasa vya maji vyenye uwezo wa kuvuta lita 3000 kwa saa, ukarabati wa vyoo pamoja na ujenzi wa vyoo bora vya mfano kwenye shule za msingi, vituo vya afya, masoko na ofisi za kata zilizopo kwenye maeneo yatakayonufaika na mradi huo.
Katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika jana eneo la Mbagala manispaa ya Temeke, mgeni rasmi, Katibu mkuu wa Wizara ya Maji Bashiri Mrindoko aliyehudhuria kwa niaba ya waziri wa maji, alisema kiasi cha fedha kilichotumika kwenye mradi huo ni kikubwa kuliko bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014, hivyo ni wajibu wa kila Mwananchi kuwa mlinzi wa mwenzake ili uweze kudumu kwa manufaa ya walengwa na taifa kwa ujumla.
Aliongozana na ujumbe kutoka serikali ya Ubelgiji akiwemo waziri wa maendeleo Peter Moors, Mwakilishi wa umoja wa nchi za Ulaya (EU) Eric Beaume, Carl Michels ambaye ni Mkuu wa BTC kutoka makao makuu nchini Ubelgiji pamoja na Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania Koenraad Adam.
Katibu mkuu huyo wa Wizara alisema elimu kwa Wananchi juu ya faida za mradi huo katika maisha yao inahitajika ili kuondoa uwezekano wa kuharibiwa kwa miundombinu ikiwemo kukata mabomba, kuibwa kwa pampu za kisasa za kuvutia maji na mifuniko ya vyoo.
Alisema Serikali imechukua jukumu la kutekeleza mradi huo ili kwenda sambamba na dira ya serikali ya maendeleo ifikapo 2025 pamoja na ile ya umoja wa mataifa (UN) ya malengo ya maendeleo ya milenia, ili ifikapo mwakani Tanzania iwe imepiga hatua kubwa kupunguza umasikini uliokithiri.
Aidha alisema waliamua kuwalenga watu walio pembeni mwa jiji kwakua hawafikiwi na huduma ya maji inayotolewa na Kampuni ya maji safi na maji taka (DAWASCO) hali inayowapa wakati mgumu kupata maji safi na salama kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Pia alisema kwa mujibu wa taarifa aliyoipata kutoka kwa mwakilishi wa umoja wa watumiaji wa maji Dar es Saalam Lydia Chagula, kuhusu tatizo la umeme kuwa mdogo kuweza kusukuma mashine kubwa za kuvutia maji, atalifanyia kazi kwa kulifikisha kwa wahusika ili utumiaji wa jenereta zinazofanya kazi muda wote kwa sasa katika visima husika usitishwe na zitumike kwa dharura mara umeme unapokosekana.
Naye Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Koenraad Adam alisema anaipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuwasaidia wananchi kuondokana na umaskini kwa kuanzisha mpango wa Matokeo makubwa sasa (BRN), hatua anayoiona kama mkombozi mwa wengi kiuchumi endapo wananchi watashiriki kikamilifu.
"Serikali inafanya kazi yake na Wananchi tunatakiwa tuunge mkono kila linalofanywa na Serikali katika juhudi za kutukwamua kiuchumi kwani bila sisi Waziri au mbunge ambaye yuko Dodoma sasa hivi kwenye bunge maalum la katiba hawezi kufanya lolote la kimaendeleo kwa nchi hii," alisema Balozi Koenraad.
Pia aliongeza, "Ubelgiji ni nchi ndogo sana barani ulaya, lakini ina baraka ya mvua karibu mwaka mzima hivyo tuna maji mengi sasa mimi pamoja na Serikali yangu tunataka kuhamishia baraka hiyo Tanzania kwa kuwasaidia kadri ya uwezo wetu ili mpate maji safi na Salama."
Kwa upande wake Mwakilishi wa umoja wa nchi za ulaya (EU) Eric Beaume, alisema Watanzania wanatakiwa watambue kuwa maji ni uhai, pia ni mali hivyo hayatakiwi kuchezewa kwasababu mara yanapokosekana maisha ya mwanadamu yanakuwa hatarini.
Mwakilishi huyo alisema mradi uliotolewa kwa Wakazi wa nje ya Dar es Saalam ni moja kati ya miradi ambayo itaendelea kutolewa na Serikali ya Tanzania, jumuiya ya nchi za ulaya na Serikali ya Ubelgiji iwapo wananchi wataonyesha ushirikiano kwa kuitunza kwa nguvu zote na akili pia.
0 comments: