Tuesday, March 25, 2014

Kawambwa : Shule za Kata ziling'ara ufaulu kidato cha nne 2013

ad300
Advertisement
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa amekanusha tuhuma zilizoelekezwa kwa Serikali kuwa haizithamini shule za sekondari za kata kiasi cha kuchangia kudhorota kwa kiwango cha ufaulu nchini kwenye miaka ya hivi karibuni.

Shukuru Kawambwa - Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Waziri Kawambwa alisema umefika wakati wa Mwananchi kutambua juhudi inazozifanya Serikali ili kuinua sekta ya Elimu katika viwango vinavyoridhisha kimataifa  na kupunguza malalamiko yasiyo na ukweli.

Alisema ni kweli Shule hizo zina changamoto nyingi lakini Serikali inazitambua na kwa kuwatumia viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia Elimu kwenye ngazi ya halmashauri wakiwemo Maofisa Elimu wanatimiza wajibu wao ipasavyo kuzibaini ili zipewe kipaumbele.

Waziri huyo alisema takwimu za matokeo ya kidato cha nne 2013yaliyotolewa na Baraza la mitihani Februari mwaka huu, zinaonesha ongezeko la ufaulu hususan kwenye shule za kata ambapo wanafunzi wengi wamepata ufaulu wenye vigezo vya kuendelea na kitado cha tano.

Alisema katika matokeo hayo jumla ya wanafunzi 74,324 waliopata daraja la 1 mpaka la tatu, 30,094 walitoka Shule za kata zinazonyooshewa vidole kuwa Serikali imezisahau, huku 10,927 wakitoka shule kongwe za Serikali na 32,324 wakiwa ni wale waliosoma shule za sekondari binafsi.

"Kwa mantiki hiyo si kweli kuwa shule za kata hazifaulishi, ni wazi zina changamoto nyingi ikiwemo vitabu na miundombinu, lakini ninawasifu walimu kwa kazi kubwa waliyoifanya, Serikali itaendelea kutatua mapungufu yaliyopo," alisema Dk. Kawambwa.

Aidha alisema sababu ya kuongezeka kwa ufaulu huo ni pamoja na mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ambao walidhamiria ufaulu uwe asilimia 60 lakini kutokana na ufinyu wa muda, wameshindwa kufikia kiwango kwa kufaulisha kwa asilimia 58.2 ngazi ya Sekondari na asilimia 50.6 kwenye matokeo ya darasa la saba.

Pia alisema uboreshwaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMEM) na ule wa Msingi (MMES) kumechangia kwa kiasi kikubwa ufaulu huo wa asilimia 43 ambao kwa mwaka uliopita ulishuka kwa kiwango cha kutisha cha asilimia 31.

Waziri alisema pia anaamini kuwa baada ya Taasisi ya Elimu kukabidhiwa dhamana ya ukaguzi wa ubora wa vitabu vya kiada, majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na EMAC, ufaulu utaongezeka zaidi kutokana na shule zote kutumia vyanzo vinavyofanana kujifunzia tofauti na ilivyokuwa awali.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: