Advertisement |
Uchaguzi huo utafanyika baada ya wajumbe kujadili na kupitisha Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, ambayo itaanza kujadiliwa Jumatatu.
Jaji Werema alitoa kauli hiyo jana alipowasilisha mada kwenye semina ya wajumbe wa Bunge Maalumu kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema ni vyema wajumbe wakaweka kando suala la itikadi, badala yake watende haki kwa kumchagua mtu atakayewanufaisha kwa kutenda haki, huku wakiweka kando rushwa.
“Nawaomba mtumie haki ya uchaguzi kwa busara. Naomba msianze mambo ya rushwa, tukianza hivyo tutaanza vibaya. Chagua mtu atakayetenda jukumu kwa haki,” alisema.
Jaji Werema pia aliwaomba wajumbe kuheshimu utaratibu na miongozo iliyowekwa, ikiwemo kuzungumza kwa zamu wanaporuhusiwa na kujenga utamaduni wa kuvumiliana wakati wa kuwasilisha hoja.
“Acheni tabia ya kila mmoja kuzungumza bila kupata ruhusa ya mwenyekiti, au kuwasha mic (vipaza sauti) kabla ya kuruhusiwa kuzungumza. Tusizungumze kama bata,” alisema.
Hata hivyo, tangu vikao vianze Jumanne wiki hii, baadhi ya wajumbe wamekuwa wakikiuka utaratibu kwa kuzungumza bila ruhusa, licha ya kupewa mwongozo wa namna ya kuzungumza ndani ya ukumbi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mwenyekiti na makamu wake, mmoja akitoka Tanzania Bara mwingine atatoka Zanzibar.
Wakati muda wa uchaguzi ukiwa bado, baadhi ya wajumbe wamekuwa wakitajwa kutaka kuwania nafasi hizo, huku wakihusishwa na kampeni za chini kwa chini.
Katika hatua nyingine, akiwasilisha mada, Jaji Werema alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, katika kifungu cha Tunu za Taifa inazuia wajumbe kufanyia marekebisho suala la Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo hoja ya serikali moja ni suala gumu.
Hilo linafanya ajenda ya serikali moja inayodaiwa na baadhi wajumbe, akiwemo Rais wa TADEA, John Chipaka, kutojadilika.
Kuhusu hoja iliyoibuliwa na wajumbe wakihoji sababu za katiba kuwa katika lugha ya Kiswahili pekee, Jaji Werema alisema itaendelea kuwa katika lugha hiyo kwa kuwa hilo linatokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Jaji Werema alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iko katika lugha za Kiingereza na Kiswahili, lakini mwongozo unaotumika ni kuwa, iwapo kutakuwepo mgongano wa tafsiri, ya Kiingereza ndiyo itatumika.Alisema kigezo hicho kimetumika kutokana na sababu za kihistoria ambazo hakuzifafanua.
0 comments: