Advertisement |
Tanzania kwa muda mrefu kumekuwa na Malalamiko lukuki kuhusu adha ya Usafiri hususani usafiri wa nchi kavu unaotumiwa na walio wengi.
Kilio hiki kiliweza kusikika kwenye Usafiri wa Mabasi ya ndani ya nchi mpaka yatokayo nje ya mipaka na Usafiri wa Reli ya Kati. Huduma bora kwa Msafiri ilikuwa tatizo kubwa kiasi cha kutishia usalama wa abiria.
Sidhani kama SUMATRA walikuwa hawalioni hili, ila nina amini walikuwa bado hawajapata njia sahihi ya kupambana na kulitokomeza kabisa tatizo hili.
Ni juzi tu, walitangaza namba ya simu ambayo Mwananchi anaweza kuitumia kuwasiliana nao moja kwa moja na kutoa malalamiko yake kuhusu usafirishaji.
Ni hatua nzuri sana kuonesha kumjali Mwananchi, badala ya kukaa kimya tu pasipo kuchukua hatua yoyote.
Kwa kitendo walichokifanya nina amini watapata si malalamiko tu, bali hata mawazo mapya kutoka kwa Wananchi, Mawazo yatakayo wasaidia kama Taasisi kuboresha zaidi huduma zake.
Kwa Utafiti mdogo nilioufanya, nimebaini Wananchi wengi wamefurahishwa na kupewa Rungu hilo japo ni wazi kuwa Namba hiyo wengi pia hawajaifahamu kutokana na ama kutangazwa kwenye vyombo vichache vya habari au kutangazwa mara moja tu pasipo kurudiwa ili kumsaidia yule ambaye awali hakusikia au ambaye hakupata chapisho la kwanza lililotolewa likiwa na habari hiyo njema.
Ni wazi kuwa SUMATRA wanatakiwa walipe uzito wa hali ya juu suala hili, kwani inaonekana wamefanya tu ili waonekane walitoa namba hiyo kama ishara ya kuwajali Wananchi.
Uwezo wanao, kwanini wasiiandike Namba hiyo ya simu kwenye kila kituo cha Mabasi madogo yanayotoa huduma mijini na vijijini na hata kwenye vituo vikubwa vya Mabasi yaendayo Mikoani na Nje ya nchi?
Nikilifikiria swali hili, narejea kwenye jambo kuu nililolisema kwenye mistari michache iliyopita kuwa SUMATRA hawajalipa uzito unaohitajika kwenye suala hili.
Ukweli ni kwamba wasafiri wanateseka sana kote nchini, kwani ni haki yao kupata huduma bora kutoka kwa wahudumu wa vyombo vya usafiri kwani wanalipia huduma hiyo, lakini hali haiko hivyo.
Kuna tabia inayofanywa na Mabasi yanayofanya safari zake kwenye miji mikubwa nchini hususani Dar es Salaam, ya kulipa nauli mara mbili kutokana na abiria kuzunguka na basi husika kabla ya kufika mwisho wa Safari kwa kukwepa vurugu pale kituoni.
Tabia hii si nzuri hata kidogo, ni uonevu wa hali ya juu! SUMATRA wanatakiwa kuliangalia hili ama kwa kuwapiga marufuku wenye vyombo hivyo vya usafirishaji wa abiria kupakia watu wa kurudi kabla ya kufika kituo cha mwisho au kuwapa nafasi wananchi kutoa maoni kama wanaridhika na hali hiyo iliyopo hivi sasa.
Sina shaka hata kidogo na utendaji kazi wa Taasisi hii muhimu, ila wanatakiwa kuzingatia kumjali zaidi Mwananchi kwa kuhakikisha hakuna Malalamiko au Manung'uniko kutokana na huduma wanaiyoipata japo ukweli ni kwamba huwezi kumridhisha kila Mtu hivyo basi yapungue kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyo sasa.
Na mwisho, Namba ya mawasiliano iliyotolewa ifanyiwe kazi, si iwepo tu na mara mtu atoapo Malalamiko yasikilizwe kisha yasifanyiwe kazi, haitapendeza na itaondoa ufanisi wao kama Taasisi na imani ya Wananchi itaondoka.
0 comments: