Tuesday, January 28, 2014

Kinondoni yatengeneza Mswada

ad300
Advertisement
BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni limetunga Mswada wa sheria ndogo zitakazo iongoza Manispaa hiyo katika shughuli zake za kila siku.

Mswada huo wenye sheria nne umetungwa na baraza hilo katika kikao cha Madiwani kilichokaa wiki iliyopita.

Ilielezwa kuwa mswada huo unatakiwa kufikishwa ngazi ya chini ya serikali ambapo Wananchi watapata nafasi ya kuzipitia wakiwa na Madiwani kwenye kata zao husika.

Ofisa Mahusiano wa Manispaa hiyo, Sebastian Mhoela alieleza kuwa Mswada huo wenye Sheria nne, Baraza la Madiwani liliamua urudishwe kwa wananchi ili watoe maoni yao kwa muda usiozidi siku 14 kisha Madiwani hao wakae tena ili kuupelka kwa Waziri Mkuu ili uidhinishwe kuwa Sheria kamili.

Mhoela alieleza Sheria mojawapo kuwa ni Sheria ya Matumizi ya Barabara za Manispaa ya Kinondoni  ya Mwaka 2014, ambayo itadhibiti uharibifu wa barabara kwa kuyazuiwa magari yenye uzito wa zaidi ya Tani 20 kupita katika barabara hizo.

Alisema Ukataji wa barabara za Manispaa kwa lengo la kupitisha Mabomba ya maji pia ni moja ya vitendo vilivyokatazwa na sheria hiyo itakayo mtaka mhusika kurudishia barabara hiyo kama ilivyokuwa awali mara atakapo pata idhini ya Manispaa kukata barabara hiyo.

Aidha, Sheria hiyo imekataza mikokoteni na Maguta kupita kwenye Barabara zote kuu za Manispaa hiyo akiziainisha Morogoro, Ally Hassan Mwinyi, Mandela na Old Bagamoyo.

Sambamba na hilo Mhoela alieleza kuwa ufungaji wa barabara za Manispaa kwa ajili ya Sherehe haitaruhusiwa na Sheria hiyo hivyo kumtaka Mhusika kutoa njia mbadala ya watumiaji barabara ili aweze kufunga barabara hiyo kwa matumizi yake binafsi.

Pia Ofisa Mahusiano huyo alitaja Sheria ya Ushuru wa Masoko kuwa mojawapo ya sheria mpya za Manispaa hiyo, ambayo itaongeza ushuru wa soko kuanzia Sh.100 iliyopo sasa mpaka kufikia Sh.300 kwa siku, ili kuboresha miundombinu na kuweka mfumo utakao wanufaisha wafanya biashara kiuchumi.

Katika Sheria hiyo, Manispaa imezuia shughuli zote za kisiasa ikiwemo kupeperusha Bendera ya Chama chochote cha siasa kwenye soko lolote lililo kwenye Manispaa ya Kinondoni na kumtaka mgombea yeyote wa nafasi ya uongozi wa Soko kuwa lazima awe Mfanya biashara.

Pamoja na hizo, Ofisa Sebastian Mhoela alisema Sheria ya Ushuru wa huduma za Jiji ambayo itamtoza mfanyabiashara asilimia 3 ya faida yake na Marekebisho ya Ushuru wa Manispaa ni sheria zingiwe zilizokubaliwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo zijumuishwe ili ziwe Sheria kamili baada ya kupitishwa na Wananchi wao na kusainiwa na Waziri Mkuu.   

Alieleza kutokana na kuwepo kwa Sheria hizo, Manispaa itamchukulia hatua mtu atakaye kwenda kinyume na Sheria hizo kwa kumtoza faini au kifungo kisicho pungua Miezi Sita. 
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: