Monday, September 30, 2013

UVCCM Arusha 'hakujatulia' bado

ad300
Advertisement
Katibu wa Tawi la Moivo wilayani Arumeru (UVCCM) Ally Shaaban Ally, amedaiwa kukamatwa na polisi akihusishwa na mauaji ya bilionea Erasto Msuya kutokana na shinikizo la kisiasa.

Habari zinasema kukamatwa kwa kiongozi huyo kulitokana na vita ya makundi inayoendelea ndani ya CCM huku yeye alikuwa akipingana na msimamo wa baadhi ya vigogo kuhusiana na uchaguzi wa mwenyekiti wa chipukizi mkoani humo uliofanyika Septemba 21, mwaka huu.

Kwenye kikao na waandishi wa habari, kiongozi huyo anayejulikana maarufu kama Majeshi alimtuhumu kigogo mmoja wa UVCCM mkoa ambaye hakumuweka wazi kuhusika na mchezo huo mchafu kwa madai kuwa kabla ya kukamatwa kwa siku moja kwenye Kituo cha Kati cha Polisi alimtishia kuwa angemfunga.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa, Duwan Nyanda ambaye pia ni Ofisa Upelelezi wa Mkoa (RCO), alikanusha Ally kukamatwa na jeshi hilo huku akiwataka waandishi kuwasiliana na kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro mahali kesi hiyo ilikofunguliwa.

Alisema kutokana na taratibu za kipolisi haiwezekani mtuhumiwa kukamatwa Arusha bila ya yeye kuwa na taarifa, hivyo akasisitiza kuwa hakuna tukio kama hilo, huku akiwataka waandishi kama hawajaridhika wawasiliane na viongozi wa CCM ili kupata ukweli.

Majeshi alisema kuwa alikamatwa kimkakati siku ya Ijumaa saa 11:30 jioni akiwa maeneo ya soko la Kilombero na kuhusishwa na kesi hiyo ili kumfanya asishiriki kwenye uchaguzi wa chipukizi wa mkoa ambapo kuna kigogo alikuwa anataka mtoto toka Wilaya ya Monduli ashinde jambo ambalo alikuwa akilipinga.

Alisema kuwa polisi watatu, wawili wakiwa wamevaa kiraia na mmoja akiwa na sare za jeshi hilo pamoja na bunduki, walimkamata wakimwambia yeye ni jambazi sugu aliyekuwa anatafutwa kutokana na mauaji ya mtu ambaye hawakumtaja jina, hivyo wakamnyang’anya simu na kuchukua vitu alivyokuwa navyo mfukoni.

Alisema kuwa alikaa kituoni hapo hadi siku inayofuata. Hakuandika maelezo yoyote zaidi ya kuandika jina, umri kabila na dini yake. Aliachiwa baada ya kudhaminiwa na Katibu Mwenezi wa CCM Arusha mjini, Gasper Kishumbue.

Kada huyo alifafanua kuwa kwa sasa anaishi kwa hofu, kwani ndugu, jamaa na marafiki wa Msuya wanaweza kupata taarifa hizo zisizo sahihi kuwa yeye alishiriki mauaji ya mpendwa wao halafu hajachukuliwa sheria, na hivyo wakamdhuru.

Katibu wa UVCCM mkoa, Salum Kidima alipoulizwa madai ya yeye kuhusika na sakata hilo, alikanusha huku akisema kuwa hana uwezo wa kulituma jeshi hilo, na kwamba taarifa alizonazo ni kuwa Majeshi alikamatwa baada ya kufananishwa na mtuhumiwa Ally Majeshi anayeishi Simanjiro mkoani Manyara.

Msuya aliyekuwa mfanyabiashara wa madini aina ya tanzanite aliuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi zaidi ya 20, Agosti 7, mwaka huu, majira ya mchana eneo la Mjohoroni kando ya barabara kuu ya Moshi – Arusha, ambapo kesi yake inaendelea.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: