Wednesday, May 16, 2018

Bil 2.8/- zawa chachu ya kuboresha elimu Lindi

Kitendo cha elimu kuonekana kuwa changamoto mkoani Lindi, serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa jumla ya Sh. Bilioni 2.8 kuhakikisha mkoa huo unashika nafasi za juu kitaifa kwenye ngazi zote.



Mbali na fedha hizo ambazo kimsingi ni za programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R), wadau mbalimbali wa elimu mkoani humo akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wamedhamiria kufufua hadhi ya mkoa huo kitaaluma.



Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Godfrey Zambi, ambaye amesema atahakikisha mkoa wake unapanda kitaaluma hasa ikizingatiwa tayari Program za EP4R na KKK zimeonyesha njia na kupokewa vizuri na baadhi ya wananchi wa Lindi.



Amesema mkoani hapa kuwa, faida za kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia shuleni ni nyingi na kwamba serikali inalitambua hilo hivyo kuhimiza wananchi kuunga mkono jitihada hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye. 



Zambi ametolea mfano shule ya msingi Mnacho, iliyopo wilayani Ruangwa, ambayo ndipo aliposomea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa awali kabla ya ukarabati, ilikuwa na hali mbaya kiasi cha kutaka kuifunga. 



"Tunaishukuru serikali kwa program zake za EP4R na KKK, ambayo inahimiza ufahamu wa kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa hatua za awali shule za msingi, imeonyesha njia ya wengine kufuata katika suala zima la maboresho ya miundombinu ya shule," amesema. 



Amesema licha ya kwamba ukarabati huo wa Mnacho haukuwa wa program ya EP4R, hali iliyopo shuleni hapo kwa sasa kama ilivyoelezwa na Mwalimu Mkuu, Theodensia Lukanga, imethibitisha kuwa juhudi za wadau binafsi kuisaidia serikali kwenye ukuaji wa sekta ya elimu zinawezekana. 



Mwalimu huyo amesema shule hiyo ilikarabatiwa kwa msaada wa wadau mbalimbali, wakishirikiana na Waziri Mkuu Majaliwa, Mkuu wa mkoa na uongozi wa serikali ya kijiji na kata, hatua iliyoifanya ionekane mpya. 



Amesema kwa ukarabati huo, wanafunzi wamepata hamasa kubwa kitaaluma na kuiomba serikali iendelee kuwatazama kwa jicho la tatu, hasa kuhusu upatikanaji wa walimu wanaokidhi uhitaji wa shule hiyo yenye historia ya kutoa kiongozi wa juu wa nchi.



Shule hiyo ya Mnacho ni moja kati ya shule za msingi mkoani Lindi, ambazo ukarabati wake haukuhusisha mradi wa EP4R lakini juhudi za wadau zimeifanya iwe na hali nzuri inayotoa fursa nyingine ya  kuandaa viongozi wengine wa kitaifa na kimataifa kwa kipindi kifupi kijacho. 

Tuesday, May 15, 2018

NIC watoa 'Support' jimboni kwa Naibu Waziri Ulega


 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Mkuranga,Abdallah Ulega akipokea mifuko 200  saruji kutoka kwa Mkurugenzi wa Masoko wa Shirika la bima la Taifa,Elisante Maleko yenye thamani ya shilingi milioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya zahanati na madarasa.
 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Mkuranga,Abdallah Ulega akipokea kava la tairi la gari kutoka kwa Mkurugenzi wa Masoko wa Shirika la bima Taifa,Elisante Maleko  leo mkoani Pwani.
 Naibu Waziri wa Mifungo na Uvuvi na  Mbunge wa Mkuranga  Uvuvi,Abdullah Ulega akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.

MBUNGE na Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi Abdallah Ulega leo Mei amepokea mofuko 200 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni tatu kutoka shirika la bima la Taifa kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati.

Akizungumza na Michuzi blog Ulega ameeleza kuwa saruji hizo zitatumika katika ujenzi wa zahanati katika vijiji mbalimbali kama Kibamba, kazole, Yavayava  na Mkanonge Wilayani humo.

Ulega ameeleza kuwa kazi hii ni yetu sote katika kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli na kuifikisha Tanzania mbele zaidi.

Pia ulega ameeleza kuwa ujenzi wa miundombinu hasa ya madarasa na Zahanati unaendelea katika vijiji mbalimbali na hii ni katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za msingi.

Aidha Ulega ameshukuru shirika hilo kwa msaada huo wa kusaidia Wilaya ya Mkuranga kwa ujenzi wa shule na zahanati.

Kwa upande wake  Meneja Masoko wa Shirika la bima la taifa Elisante Maleko ameeleza kuwa utoaji wa mifuko hiyo ya saruji ni kutokana na mahusiano mazuri baina yao hivyo wakaona faida wanayopata kutoka kwa wananchi hao ambao ni wateja wazuri ni kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya madarasa na zahanati katika vijiji mbalimbali vya Mkuranga.

Mkurugenzi wa Shirika hilo tawi la Ubungo Segeja Mabulla amemshukuru mbunge na mkuu wa wilaya hiyo kwa kuwakutanisha na kutoa elimu ya kuwasaidia wananchi kuhusiana na masuala ya bima pia amewapongeza wakazi wa Wilaya hiyo kwa kuwa wateja wazuri wa bima za halmashauri na bima za maisha.

Saturday, April 21, 2018

Kibaha Sekondari kidedea uandishi wa Insha

Kibaha Sekondari kidedea uandishi wa Insha

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu,  amezitaka Shule za Sekondari nchini ambazo zimekuwa zikishindwa katika mashindano ya insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika SADC kujifunza kupitia shule ambazo zimekuwa zikifanya vizuri.

Dk. Semakafu ameyasema hayo mjini Dodoma wa wakati hafla ya kuwazawadia washindi wa insha hizo kwa mwaka 2017 ambapo amesema ni vema kukawa na  utaratibu wa kuzikutanisha shule hizo mara moja kwa mwaka ili kujadiliana mbinu mbalimbali zitakazowawezesha kufanya vizuri katika mashindano hayo. 

Semakafu amesema ushindi huu ni dhahiri kuwa Elimu  inayotolewa nchini  ni Elimu bora na ndiyo maana wanafunzi wa kitanzania wameweza kushinda tuzo na kuongoza  katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za kusini mwa Afrika.

Afisa Elimu Mkuu wa sekretaieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, James Otieno,  aliiunga mkono  kauli hiyo kwa kusema kuwa Elimu nchini Tanzania ni bora kwa Nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwsababu wanafunzi kutoka Tanzania wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano hayo.

Kwa upande wake Mwanafunzi bora wa mashindano ya insha hizo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Michael Msafiri kutoka Shule ya Sekondari Kibaha ndiye atakuwa mwakilishi wa washindi wote katika Mkutano Mkuu wa Wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo utakaofanyika baadae mwaka huu mkoani Arusha.

Kaimu Mratibu wa mashindano hayo Salum Salum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema mshindano haya huanza mara baada ya kikao cha wakuu wa Nchi wanachama kutoa azimio la mwaka na kwamba mada zinazoshindanishwa huzingatia makubaliano ya wakuu wa nchi.

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI, NA TEKNOLOJIA.
18/4/2018

Sunday, April 15, 2018

Kodi kutozwa kwa watumia mitandao ya kijamii

WAZIRI wa Fedha wa Uganda Matia Kasaija ameliambia Shirika la Habari la Uingereza Reuters kuwa serikali yake inapanga kuwatoza kodi watumiaji wa mitandao ya kijamii kila siku, kuanzia Julai mwaka huu, hatua inayolenga kuisadia serikali kukusanya mapato.
“Tunahitaji fedha za kuisaidia kuimarisha usalama, kuweka miundo mbinu ya umeme na mambo mengine muhimu,” alisema.
Hata hivyo, wanaharakati wamepinga mpango huu kwa kile wanachosema ni mpango wa serikali ya rais Yoweri Museveni kuminya uhuru wa kujieleza.
Watumiaji wanatarajiwa kutozwa Shilingi za Uganda 200 au 100.
Mapema mwezi huu, rais Yoweri Museveni alimwandikia barua Waziri Kasaija na kumwagiza kuja na mbinu za kukusanya fedha kutoka watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Museveni ambaye amekuwa akiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 30 sasa amesema Mamilioni ya raia wa Uganda wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kusambaza habari za uongo.
Hata hivyo, mpango huu hautawaathiri wanaotumia mitandao hiyo kwa ajili ya masuala ya elimu.
Wanasiasa wa upinzani nchini humo wamesema hiyo ni njia ya rais Museveni kuonesha kuwa anaogopa ushawishi wa mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter.

Saturday, April 14, 2018

FCC yawanoa wadau wa biashara, viwanda

WIZARA ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imesema wafanyabiashara na wenye viwanda nchini, wanapaswa kufuata utaratibu katika uwasilishaji malalamiko, mapendekezo kuhusu usimamizi wa sheria za biashara badala ya kulalamikia pembeni.



Imesema usimamizi wa sheria zikiwemo zinazohusu usimamizi wa soko, upo kisheria licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa sambamba na faida, lakini msingi wa maendeleo kwenye mataifa yote duniani unaanzia kwenye utekelezaji mzuri wa sheria na usimamizi wa soko.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Aristides Mbwasi, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante Ole Gabriel, kwenye ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa biashara nchini kilichoandaliwa na Tume ya Ushindani (FCC).

Akisoma hotuba ya katibu mkuu, Aristides amesema Tume ya Ushindani ni chombo muhimu kilichoanzishwa ili kusimamia utendaji na ufanisi wa mfumo wa soko hapa nchini, hivyo wafanyabiashara ni miongoni mwa wadau wakubwa wa taasisi hiyo.

Hata hivyo, amesema wakati wa utekelezaji wa majukumu yake, inawezekana kukatokea malalamiko kutoka kwa upande wa pili, ambapo ili kupata ufumbuzi hakuna budi pande zote zikaa na kuzungumza kwa utaratibu uliowekwa.

Amesema semina za kuelimishana na kushauriana kama ambayo aliifungua jana, ni njia mojawapo ya kuwakutanisha pande tofauti tofauti na kuzungumza yanayowahusu kwa lengo la kutoka na msimamo mmoja wenye lengo la kujenga.

"Wasilisho lenu kwenye semina hii linaweza kuboresha miundo ya kisera na kisheria kwa kuwa zote zinaweza kurekebishwa lakini kwa kuzingatia maslahi ya walaji na watumiaji ambao ni wananchi na uchumi kwa ujumla," amesema kwenye hotuba hiyo.

Ameongeza kwa kutoa rai kwa vyombo vingine vya serikali vilivyohudhuria semina hiyo ikiwemo TFDA, TBS, BRELA, TAFFA, TPSF, CTI na Maofisa biashara wa wilaya na mikoa kuangalia namna bora ya kushirikiana na wafanyabiashara, wenye viwanda katika kutekeleza sheria zinazohusu usimamizi wa soko nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Dk. John Mduma, amesema semina hiyo ni katika kutekeleza azma ya tume hiyo ya kuwaelimisha wadau mbalimbali kupitia vyama na jumuia zinazowaunganisha juu ya shughuli inazozifanya kisheria ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji wa pande hizo.

Amesema wanatarajia kuitumia semina hiyo kushauriana na wadau na kuelekezana kuhusiana na masuala mbalimbali ya udhibiti wa bidhaa bandia, ili kuimarisha mahusiano chanya  ambayo ni muhimu kwenye usimamizi wa shughuli za kibiashara katika mfumo wa uchumi na soko.

Dk. John amesema pia ili kuwa karibu zaidi na walaji, wameamua kuweka wazi namba ya simu ya bure, ambayo jana ilizinduliwa rasmi, itakayokuwa maalumu kwa wateja kuishauri FCC au kulalamika juu ya changamoto za sokoni.

Namba hiyo ni 0800110094.

Friday, April 13, 2018

Simu inasababisha saratani?

"Usiweke simu karibu na unapolaza kichwa chako usiku, ni hatari kuna mionzi itazuru ubongo wako na utapata saratani ya ubongo, ukipata meseji hii mtaarifa na umpendaye... Mimi nimeanza na wewe!

Niambie, umewahi kupata ujumbe wa namna hii kwenye simu yako ya mkononi tena kwa mtu unayemjua kabisa anaweza kuwa ndugu, rafiki au hata jirani? Bila shaka jibu litakuwa ndio kuonyesha kukubali na inawezekana nikikupa nafasi ya kujieleza ukaniambia "Si mara moja."

Hizi kimsingi ni baadhi ya jumbe ambazo watumiaji wa simu za mkononi huzisambaza kwa mtu au watu kwa mfumo maarufu unaoitwa "Copy & Paste" kwa sababu ameipokea kwa mtu A akaona una manufaa japo hajiulizi kama una ukweli wowote au lah, yeye huamua tu kutuma kwa mtu B au mara zingine mtu C, D na hata F.

Jumbe hizi huleta hofu kwa mwingine, licha ya kwamba mtumaji alikuwa na nia njema lakini haweza kufanya aliyepokea akaanza kuiogopa simu yake kwa kigezo tu cha kuwa mbali na majanga ya kupata saratani ya ubongo.

Ni wazi kuna aina lukuki za saratani kwa miaka ya hivi karibuni ikilinganishwa na miaka 50 iliyopita na ukweli ni kwamba saratani yoyote ile inatisha kwa sababu kwa mujibu wa madaktari na wataalamu wengine wa utafiti wa afya za binadamu, bado haina tiba, mionzi hufanya kwa kiasi tu japo watu hupona kwa imani za kiroho.

Hoja ya simu za mkononi kusababisha saratani kutokana na madai kuwa zina mionzi mikali inayodhuru ubongo wa binadamu ni ya muda mrefu, sijaona utafiti wowote uliofanyika kufikia muafaka huo kwa sababu nimepekua maeneo mengi bila mafanikio zaidi ya kupata majibu ya tafiti zinazoangalia kuhusu kukanusha madai hayo.

Kwa maana hiyo utafiti upo, hata kama ulifanywa kwa kiwango kidogo au sampuli ndogo, kwa kitendo cha mimi kuona tu utafiti huu mpya naamini wapo watu walichunguza na kubaini ukweli kuwa simu za mkononi husababisha saratani; kwani utafiti hupingwa na utafiti huu ndio ukweli.

Utafiti huu niliouona imefanywa na kusimamiwa na Shirika la Marekani linalosimamia Chakula na Dawa FDA, (ambayo ni taasisi kama ilivyo TFDA hapa nchini) kwa kushirikiana na Mpango wa kitaifa nchini humo unaohusika na masuala yanayohusu sumu (National Toxicology Program).

Kwa maelezo yao, simu ya mkononi ili kuweza kuwasiliana na mtandao wa mawasiliano kuna miyonzi ambayo inakuwa inatoa au kuzalisha mionzi inayojulikana kama Radiofrequency.

Mionzi hii inatajwa kuwa haina ukali mkubwa kama mionzi inayotolewa na vipimo vya X-ray ambavyo vinatoa mionzi inayotambulika kama ionizing yenye uwezo wa kupenya nyama na kufikia mifupa ya mwanadamu huku ikiua baadhi ya seli.

Wataalamu wa afya wanasema vifo hivi vya seli ndivyo kitaalamu husababisha saratani pale ambapo vitendo vya tiba vinapotoa mrejesho hasi.

Nini kilifanyika?

Kwenye utafiti huo kundi la panya liliwekwa kwenye mazingira yaliyozungukwa na mionzi ya radiofrequency muda wote na kiwango cha mionzi hiyo kiliwekwa juu kuzidi hali ya kawaida ya mionzi inayotolewa na simu tunazozitumia.

Moja ya matokeo ya utafiti huo yalionesha panya wa kiume ndio waliathirika zaidi, ambapo walipata uvimbe fulani ulioanza kukua maeneo ya mioyo yao.

Panya wa kike ambao pia walikuwa kwenye eneo hilo hilo hawakupata madhara yoyote hasi yaliyoonekana na wataalamu hao lakini jibu la mwisho likawa uvimbe kwenye mioyo ya panya dume haikuwa aina yoyote ya saratani.

Wataalamu hao walikwenda mbali zaidi ya utafiti wao kwa kuwafuatilia kwa ukaribu panya wote baada ya kukamilisha utafiti wao ambapo walibaini wale ambao walikuwa kama sampuli ya utafiti waliishi umri mrefu zaidi ikilinganishwa na jamii ile ile kwa ambao hawakuguswa kabisa na jaribio hilo la kitaalamu. Hawakutoa majibu kwanini hali hii ilitokea!

Tunafahamu kwamba kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna mifumo mbalimbali ya mawasiliano ya simu ikiwemo 2 generation au kwa kifupi 2G (Edge), 3G, 4G na kwa wenzetu walioendelea wameshafika 5G sasa panya hao waliwekwa kwenye eneo lililofungiwa kiwango cha juu cha mionzi ya radiofrequency katika mfumo wa 2G na 3G.
Waliishi kwenye eneo hilo kwa muda wa miaka miwili ambayo kwa makadirio ya kitaalamu umri wa miaka miwili wa panya ni takribani miaka 70 ya mwanadamu.

Angalizo walilolitoa wataalamu wale ni kwamba "Matokeo ya utafiti huo yasihusishwe moja kwa moja na madhara yanayoweza kutokea kwa utumiaji wa simu wa mwanadamu kwa sababu panya hao waliwekwa kwenye kiwango cha juu sana cha mionzi kuliko kiwango cha kawaida kinachotolewa na simu."

Kiuhalisia ni sentensi niliyoitafsiri kwa ufasaha kabisa kutoka lugha ya kiingereza kuja kiswahili lakini bado inaonekana kuwa ngumu kueleweka, si ndio? Sasa akili kichwani mwako, bora nusu shari kuliko shari kamili kwa sababu nilizungumza jana kwenye safu hii hii kuwa matumizi yoyote ya kitu chochote ni hatari hivyo tutumie vifaa hivi kwa kiasi.

Utafiti huu kwa ufupi umebainisha hakuna madhara ya kiafya kwa watumia simu, lakini wanaweza kuja watafiti wengine wakasema utafiti wao umebaini kuna madhara makubwa tena sana kiafya kwenye matumizi ya simu, chonde chonde nisionekane muongo katika hili.

Utaratibu mzuri wa kuendesha gari ya 'Automatic gear'

KWA dereva yeyote, ni wazi hawezi kupingana na mimi kwamba gia ni eneo muhimu sana kwenye gari ambalo limeundwa kwa makusudi ya kutoka sehemu moja kwenda nyingine yaani kuwa na mwendo.

Gia ndio inayofanya gari itembee kwa mwendokasi mkali au mdogo kadri dereva atakavyoamua kufuatia ubadilishaji wake wa gia akiwa kwenye mwendo.

Kitendo cha kubadili gia, kutokana na utafiti wa kitaalamu kwa baadhi ya madereva kilionekana kuwa changamoto ambapo wengi walionekana kuiumiza gari kwa kutembelea gia ambayo haikustahili kutumika kwa eneo na wakati husika.

Ni kutokana na majibu hayo ya utafiti na maendeleo ya sayansi na teknolojia wataalamu waliona badala ya kumpa shida dereva kubadili gia mara anapokuwa akiendesha gari wakaamua kuunda mfumo wa gia ambao gia zinajibadilisha zenyewe yaani automatic driving.

Kimsingi katika gari za AUTOMATIC kuna gia ambayo ina alama zinazosomeka L, 2, 3 na O/D.

Napenda ufahamu  kuwa katika hali ya kawaida wakati unaendesha gari yako inapaswa kuwa katika gia ‘’D’’ kwa maana ya ‘’DRIVE’’ na hii inategemeana na mazingira ya barabara na kama kuna hali yali ya hewa nzuri.

Gia 2 na 3 hutumika tu pale unapokuwa ama unashuka au unapanda mlima/mteremko mkali sana na mrefu mfano Sekenke, Wami au Kitonga na unataka ushuke au upande kwa spidi ile ile ila isizidi 40/60.

Namba 2,3 na L kwenye gia yako inamaana kuwa ina inazuia 'gear box' ili gia zisibadilike (-/+) kama ambavyo zinabadilika ukiweka D na itambulike kuwa unaweza kubadili kutoka D kwenda 2 au 3 wakati wowote gari inapokuwa katika mwendo.

Hata hivyo kuna tahadhari kwamba ukitaka kufanya hivyo, hakikisha usiwe spidi zaidi ya 60, kwa sababu kinachofanyika ni kwamba D inasababisha sahani (disks) zilizomo ndani ya 'gear box' kufanya kazi na hii husababisha ile hydrolic 'mafuta ya kulainisha gia' yaliyomo ndani kupata joto.

Joto hilo hutoka katika zile sahani ambapo mwisho wake joto lile husababisha gear box kutokuwa na nguvu ile ile (constant velocity) na ndio maana ukiweka namba 2, 3 au L, gear box inakuwa kwenye 'lock' na sahani hazisuguani kwa sababu inakuwa inatumika sahani/disk moja tu kwa hiyo inasaidia ile hydrolic kupoa na kufanya gari iongeze nguvu kwa ghafla.

Gia L inatumika pale unapokuwa ama umekwama au unavuta gari jingine ila inapaswa itumike kwa muda mfupi sana maana ina nguvu kupita kiasi na pia inaongeza ulaji wa mafuta.

Hivyo kama ukitoka katika mkwamo na unaona bado barabara si nzuri  labda ina utelezi au unavuta mzigo kwa mwendo mrefu basi unaweka 2 au 3 na wakati huo huo unaweza kuweka hata D kama hali ya njia na mzigo vinaruhusu.

Ukiwa katika hali hiyo unaweza kuongeza walau mpaka spidi 60 au zaidi kama utaweka D kwa maana rahisi zaidi kwamba gia namba 2,3 na L zinafanya kazi kama gari ya Manual nikimaanisha ile isiyo ya automatic na hii inakuwa rahisi kwa yeyote ambaye anafahamu kuendesha manual.

OVER DRIVE (OD) inatumika pale gari inapokuwa spidi zaidi ya 60/80 kutegemea na aina ya gari na hili hutokea bila wewe kujua maana gari yenyewe ndo inafanya ndio maana unashauriwa iwe ON muda wote kusudi gari ichague ni wakati gani iweke ON au OFF.

Kumbuka ukiwa chini ya spidi 60 hata kama umeweka ON bado inakuwa haifanyi kazi, ndivyo walivyoiunda wataalamu na hayo ndio maajabu ya teknolojia tunayoyazungumzia.

OD unaweza kuitumia kama breki ya ghafla au stop engine hasa unapokuwa zaidi ya spidi 80 na wakati huo iko ON yaani katika dashboard taa ya OD unapaswa kuwa imezima kwa sababu ikiwaka maana yake iko OFF, ukiona hivyo basi ili upunguze mwendo kwa haraka unachofanya ni kuweka OFF na wakati huo unakanyaga breki taratibu.

Kwa kitendo hicho ambacho kinatakiwa kuwa cha haraka utaona gari linavyopunguza mwendo taratibu na wakati mwingine si lazima ukanyage breki, iweke OFF halafu toa mguu katika pedali ya mafuta gari lazima ipunguze mwendo yenyewe na kama ilikuwa ni tuta na umeshalipita basi iweke tena ON, ongeza mafuta au unaweza kuweka 2 au 3 ili gari ianze kwa kasi zaidi.

Baada ya  kuchanganya basi rudi kwenye D na endelea kama kawaida na kuliongoza gari lako kwa umakini na usalama wa hali ya juu.

Tahadhari

Kamwe usikate kona wakati uko spidi kubwa na gia namba tano (MANUAL) au rpm iko 3000 (AUTOMATIC), hii husababisha kupitiliza au gari kuanguia kwa sababu katika hali hii gari inakuwa nyepesi sana.

Hakikisha umepunguza mwendo mpaka gia namba nne na kanyaga breki kidogo kama unatumia gari yenye mfumo wa manual ambao unakukazimu ufanye kila kitu ikiwemo kubadili gia na Kwa AUTOMATIC weka gia namba  2 au 3 ila lazima OD iwe OFF na uwe umekanyaga breki kidogo.