Saturday, March 3, 2018

Wakandarasi 4,000 wafutiwa usajili

ad300
Advertisement
Bodi ya Usajili Wakandarasi (CRB) imesema imewafutia usajili wakandarasi 4, 000 kutojana na sababu mbalimbali ikiwemo uvunjifu wa kanuni za bodi hiyo na kushindwa kulipa ada zinazotakiwa.

Imesema hatua hiyo ni ya mwisho kwenye kanuni za CRB zinazohusika na kumchukulia hatua mwanachama wake baada ya kutanguliwa na adhabu ndogo zikiwemo onyo na faini.

Hayo yalisemwa jana na Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo Joseph Tango, alipokuwa akizungumza mbele ya Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso, aliyekutana na wajumbe wa bodi hiyo jijini Dar es Salaam.

Alisema bodi hiyo mpaka sasa ina takriban wanachama 9,000 ambao kulingana  na majukumu ya CRB wanasimamiwa kwenye utendaji kazi wao na kuendelezwa kitaaluma pale inapohitajika.

Joseph alisema pale inapotokea mkandarasi fulani akakiuka kanuni, kuvunja sheria au kwenda kinyume na maadili ya kazi yake ikiwemo kuhujumu miradi mbalimbali anayopewa kusimamia CRB humshughulikia. 

Kauli hiyo imekuja kufuatia maneno ya naibu waziri Aweso aliyesema kwa muda wote tangu kuteuliwa kwake kwenye nafasi aliyopo sasa amekuwa akifanya ziara maeneo mbalimbali nchini kujiridhisha kuhusu utendaji wa wakandarasi wa miradi ya maji. 

Alisema kwa masikitiko makubwa miradi mingi ambayo licha ya kuwa serikali tayari imelipa asilimia 95 ya fedha zote, bado haitoi maji kama yalivyo makubaliano huku wakandarasi wakuu wa miradi ile wakiwa ni wazalendo. 

"Nimetumia muda mwingi wizarani kutembelea miradi yetu ya maji nchi nzima, inasikitisha kwamba baadhi ya wakandarasi wanafanya ujanja ujanja kwenye miradi yetu. 

" Mingi licha ya kwamba serikali tayari tumekuwa tumeshalipa fedha kwa kiasi kikubwa tu bado upatikanaji wa maji ni tatizo na hii yote unakuta inasimamiwa na wakandarasi wakitanzania. 

Aliongeza: "Baada ya kuona hivi nikasema badala ya kulalamika ngoja niende kwa baba zao ambao ni bodi ya usajili wakandarasi niseme ili ikiwezekana hawa wanaotuhujumu wawashughulikie, ndio sababu leo niko hapa ofisini kwenu." 

Pia alisema licha ya uwepo wa wakandarasi wachache wasio waaminifu, wapo wengine wanaofanya kazi nzuri kwenye miradi ya maji nchini ambapo aliiomba bodi hiyo kuhakikisha inawafikiria katika suala zima la kuwaendeleza na serikali itaendelea kuwapa kazi nyingi zaidi.

Kutokana na kauli hiyo, makamu mwenyekiti wa CRB alimuhakikishia naibu waziri kuwa wanachama wao ni waadilifu lakini kama wapo wanaorudisha nyuma jitihada za serikali katika kuwapatia maji wananchi, akabidhi majina yao na bodi hiyo itawachukulia hatua.

"Naibu waziri tunayaomba majina ya hao wakandarasi na ninakuhakikishia tutawachukulia hatua kama zilivyo kanuni zetu kwa sababu sote tunaona jitihada ambazo serikali inazifanya mijini na vijijini katika suala zima la upatikanaji wa maji," alisema.

Kwa mujibu wa CRB, wizara ya maji na umwagiliaji ni mdau mkubwa kwa wanachama wake kutokana na kuwapa kazi nyingi wakandarasi wa ndani huku wizara nayo ikisema inafarijika kuona wakandarasi hao wanajitoa kufanya miradi hiyo ikamilike kwa wakati ikiwa na ubora wa viwango vya kimataifa. 
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: