Advertisement |
Vyombo
vya habari nchini vimetajwa kuwa kiungo muhimu kwa maendeleo ya taifa
kiuchumi hasa pale vinapoendelea kutumia nafasi zao vizuri kwenye
kuhabarisha umma kuhusu kazi kubwa inayofanywa na serikali kwenye sekta
ya fedha, biashara na uchumi.
Naibu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)- Utawala na Udhibiti wa Ndani, Julian Banzi alibainisha hayo alipozungumza kwenye uzinduzi wa
warsha ya wanahabari wa biashara, fedha na uchumi mkoani Mtwara.
"Mna
nafasi muhimu kwenye kuisaidia nchi yetu hivyo ni vizuri badala ya
kutumia muda mwingi kutumika vibaya ili kuwa chanzo cha kupiga vita
jitihada nzuri zinazofanywa na serikali kwenye kuliletea taifa maendeleo
endelevu mkaamua kushirikiana na wataalamu wa BoT kujua ukweli na
kuuandika," alisema.
Gavana
huyo alisema ni wazi kuwa vyombo vya habari vimeendelea kufanya kazi
nzuri kwenye kuhabarisha umma wa watanzania juu ya maendeleo ya kiuchumi
hasa wakati huu ambao taifa linauendea uchumi wa kati ifikapo 2025.
Alisema
kasi ya kutekeleza wajibu huo haipaswi kupunguzwa bali iongezwe huku
pia weledi, ufanisi kwenye uhabarishaji huo vikipewa kipaumbele na
wanahabari wote ili kuwe na manufaa chanya badala ya upotoshaji.
"Ninawaomba
wanahabari tusitumike kuhujumu jitihada za serikali, tutumie vizuri
kalamu zetu lakini pale ambapo pana uozo wenye athari mbaya kwa
maendeleo ya taifa letu kiuchumi hamna budi kuuibua," alisisitiza Banzi.
Alifafanua
kuwa yapo mambo mengi ambayo serikali inayafanya kwa sasa na yana
manufaa makubwa kwa maendeleo ya Tanzania pale itakapokamilika, hivyo ni
muhimu vyombo vya habari vikayaeleza kwa umma ili kila mtu ajue
serikali inafanya nini kwa ajili yake na vizazi vyake.
Banzi aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi
mikubwa ukiwemo wa reli ya kisasa (SGR), Stingler Gorge na ujenzi wa
bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Tanga.
"Yote
haya yanawasubiri ninyi muwaambie wananchi umuhimu wake kwao, fanyeni
hivyo kwa sababu kuna muda mnaandika na kutangaza mambo yanayovunja moyo
kweli," alisema.
Naibu
Gavana huyo pia alitumia fursa hiyo ya kufungua semina ya wanahabari
kuwaambia kuwa BoT inafuatilia kwa karibu taarifa zote zinazohusu
masuala ya kiuchumi, biashara na masoko na kwamba wanafurahishwa na
namna ambavyo wanahabari wengi wanajitahidi kuripoti kwa usahihi.
Awali,
Mkuu wa Idara ya Uhusiano, Mawasiliano na Itifaki wa BoT Zalia Mbeo,
alisema warsha ya mwaka huu ya wanahabari wa uchumi na fedha ni ya tano
mfululizo na tayari wamepata mafanikio makubwa kwenye kujenga mahusiano
mazuri baina ya vyombo vya habari na taasisi hiyo kubwa ya kifedha
nchini.
Mafaniko
mengine aliyoyataja kupatikana kutokana na utaratibu wao wa kutoa
mafunzo ya kila mwaka kwa wanahabari alisema ni kupunguza upotoshaji wa
kitakwimu na maelezo mengine kwenye habari za kiuchumi ambazo awali
zilikuwa zikionekana kwa kiasi kikubwa.
0 comments: