Advertisement |
Hatimaye Serikali imefunga rasmi mjadala kuhusu umiliki wa ardhi eneo la hifadhi
ya msitu wa Kazimzumbwi kwa kuwaamuru wananchi waliovamia eneo hilo
kuondoka haraka.
Uamuzi
huo umetolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii
kufuatia kesi ya msingi iliyokuwa imefunguliwa Mahakamani na wavamizi
hao dhidi ya Wizara hiyo, kuamua wananchi kuhama eneo hilo la hifadhi.
Hatua hiyo inakuja huku kukiwa na wimbi kubwa la uuzaji wa viwanja unaofanywa na wavamizi ndani ya msitu huo kwa
wananchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Meneja Mawasiliano wa Wakala wa
Huduma za Misitu (TFS), Glory Mziray, aliwataka wananchi kutonunua viwanja hivyo sambamba na kutofanya shughuli
za kibinadamu ndani ya msitu huo.
Glory alisema wananchi watakaonunua viwanja ndani ya msitu huo
watahesabika kuwa wavamizi na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa vile
msitu huo umehifadhiwa kisheria.
Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayenunua kiwanja na kuanzisha makazi ndani msitu huo endapo utanunua ujiandae kuondolewa mara moja," alisisitiza.
Pamoja na hayo alisema kutokana na uharibifu unaoendelea kufanywa katika msitu
huo, tayari serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi za kuunusuru msitu huo ili
usiweze kutoweka kabisa.
Moja ya jitihada hizo alisema ni utaratibu wa kuweka vipimo vya kisasa katika msitu huo ili kuweza
kuunusuru na uvamizi pamoja na uharibifu unaofanywa na wananchi.
Alisema msitu huo umekuwa kwenye mgogoro tangu
mwaka 1998 kutokana na kuwa karibu na makazi ya watu jambo
linalochangia wakazi hao kuingia katika msitu kufanya shughuli za kibinadamu.
Migogoro
hiyo iliyohusisha wananchi na walinzi wa msitu huo, ulikuwa ukichukua
sura mpya kila mara, huku wananchi wakidai wana haki ya kuwepo eneo hilo
na kuomba viongozi wa juu wa serikali kuwasaidia kwenye utetezi.
Msitu wa Kazimzumbwi una
ukubwa wa hekta 4,860, ambapo ulitangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali (GN 306) mwaka 1954.
Uwepo wake kwenye sehemu ya wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani na wilaya ya Ilala mkoani Dar es
Salaam, msitu huo umetumika kuvuta hewa chafu kutoka katika jiji la Dar es
Salaam.
Imeandikwa na Lusungu Hellela wa Wizara ya Maliasili na Utalii na kuhaririwa na Shechambo Blog.
0 comments: