Tuesday, September 19, 2017

Mradi wa LANES washika kasi kuboresha elimu awali na msingi nchini

ad300
Advertisement
Serikali imefanikiwa kuchapisha na kusambaza vitabu zaidi ya milioni 14 kwenye shule zote za msingi za mikoa yote 26 ya Tanzania bara.

Vitabu hivyo ni asilimia 32.8 ya malengo makuu ya kusambaza vitabu zaidi ya milioni 44 vya elimu ya awali na msingi kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu, ambavyo vinatolewa kupitia Program ya Ufundishaji na Ujifunzaji (LANES).

Akizungumza mjini Dodoma jana, Mratibu Msaidizi wa mradi huo, Issack Kitururu, alisema hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwa serikali ya Tanzania na kwamba bado wanaendelea ili kufikia asilimia 100 ya usambazaji huo ifikapo Desemba 2018.

Kitururu alisema mafanikio hayo yanatokana na uhalisia kuwa hii ni mara ya kwanza tangu nchi ipate uhuru, kutekeleza mradi huo wenye nia ya dhati kupunguza na hatimaye kumaliza changamoto ya wanafunzi kutokujua kusoma na kuandika.

Mratibu huyo alisema, awali kulikuwa na tatizo la wanafunzi kufika mpaka darasa la nne au la tano bila kuwa na ufahamu wa kusoma na kuandika tatizo ambalo kutokana na mradi wa LANES, linazidi kupotea.

Alisema vitabu hivyo ambavyo vimefuata mtaala wa sasa ulioboreshwa, vimetolewa na vitaendelea kutolewa kwenye halmashauri zote nchini hadi Juni 2018, ambapo mradi wa LANES utafikia ukomo wake.

"Mradi huu pamoja na mambo mengine ikiwemo mafunzo ya walimu, unawezesha usambazaji wa vitabu kupitia Ubalozi wa Sweden hapa nchini na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI tunasimamia utekelezaji wake ipasavyo," alisema.

Aliongeza kuwa vitabu husika pia vinajumuisha vya elimu maalumu, ambavyo vinawagusa wenye usikivu hafifu, uoni hafifu na mtindio wa ubongo ili kutekeleza kwa vitendo zana ya elimu jumuishi.

Pamoja hayo, alisema usambazaji wa vitabu hivyo na matumizi yake tayari umeonyesha mafanikio makubwa kwenye maendeleo ya watoto kitaaluma hasa kwenye suala zima la kusoma, kuandika na kuhesabu yaani (KKK).

Alifafanua kuwa maendeleo yalitokana na yanayofanywa na mradi huo wa LANES, ambapo yalithibitishwa na USAID kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye kuboresha elimu ya awali na msingi kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni kuanzia mwaka 2016.

Mradi wa LANES unaojumuisha mafunzo ya walimu, uchapaji, usambazaji wa vitabu na ujumuishaji jamii kwenye masuala ya kusoma na kuhesabu, unawalenga wanafunzi kuanzia miaka mitano mpaka 13, ukiwa na ufadhili wa Dola za marekani milioni 94.8.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: