Advertisement |
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao Dkt. Vicensia
Shule (kushoto) wakati wa sherehe za uzinduzi wa Tamasha la Jinsia
lililoandaliwa na TGNP Mtandao.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akipokea tuzo ya Uongozi kwa kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza Mwanamke na
kutambua mchango wake katika kusimamia na kuhamasisha usawa wa kijinsia
na uwezeshaji wanawake kutoka kwa mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao
Dkt. Vicensia Shule (kushoto) wakati wa sherehe za uzinduzi wa Tamasha
la Jinsia lililoandaliwa na TGNP Mtandao. (Picha na Ofisi ya Makamu wa
Rais)
**************************************
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo
amezindua Tamasha la 14 la Jinsia lililoandaliwa na TGNP Mtandao.
Makamu
wa Rais amesema Serikali imechukua hatua mbali mbali ili kumuwezesha
mwananke kujikomboa kiuchumi, ikiwa pamoja na kuanzisha Benki ya
Wanawake Tanzania, kuanzisha mifuko mbali mbali ya uwezeshaji ukiwemo
mfuko wa Maendeleo ya Wanawake pamoja na kuhamasisha uanzishwaji wa
SACCOS, VICOBA na vikundi vingine vya kiuchumi.
Amesema pia serikali iliagiza asilimia 30 ya zabuni za serikali zipewe wanawake, vile vile iliagiza
halmashauri zote kutenga asilimia 5 ya mapato kwa ajili ya mfuko wa
maendeleo ya wanawake.
Samia alisema: “Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini
umuhimu wa uzingatiaji wa masuala ya jinsia katika kuchangia na
kuharakisha maendeleo ya nchi”.
Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau wa maendeleo kushirikiana
katika kuhakikisha Tanzania kama nchi inafikia lengo namba 5 la ajenda
ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya mwaka 2063 ya Afrika ya kuhakikisha Mwanamke ana haki sawa na mwanaume katika Nyanja zote za kijamii na haachwi nyuma kwenye maendeleo.
Makamu
wa Rais alisisitiza ni muhimu kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali,
Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuzingatia
vipaumbele vya kijinsia kwenye mipango yake ya bajeti.
Alisema ili kufikia usawa wa kijinsia lazima mwanamke apewe mbinu za kumuezesha kiuchumi na lazima alindwe na vitendo vya ukatili wa kijinsia ili aweze kusimama imara kwenye majukumu yake mbali mbali.
Makamu wa Rais alihimiza pia Wanawake kusaidiana na kuinuana ili kufikia malengo huku akiwapongeza TGNP na Kamati ya Kitaifa ya kuweka
kumbukumbu za wanawake kwa ajili ya kuwatambua, kuwaenzi na kuweka
kumbukumbu za michango ya wanawake katika nyanza mbali mbali za
maendeleo.
0 comments: