Advertisement |
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa
Makame Mbarawa, amewasha moto kwa wafanyabiashara waliopangisha kwenye
majengo ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, kwa
kuwapa siku 40 za kulipa madeni yao yote ya pango.
Ametoa
agizo hilo alipofanya ziara kiwanjani hapo na kuzungumza na
wafanyabiashara ambapo alisema pamoja na malipo hayo, serikali itapitia
upya mikataba na kufanya marekebisho inapohitajika.
Waziri
Mbarawa alisema serikali ina malengo mengi kwenye kuongeza ufanisi wa
viwanja vya ndege na sekta ya usafiri wa anga kwa ujumla lakini ni aibu
kwamba kila fedha lazima itoke serikali kuu.
"Tunasema
hivi kwa sababu kwa viwanja vitatu yaani hapa Julius Nyerere, KIA na
kile cha Mwanza kwa mwaka vinakusanya takriban Sh. Bilioni 60 au 70
hivi, wakati tuna uwezo wa kifika Bilioni 150 kwa mwaka, " alisema.
Alisema
viwanja vingi kikiwemo cha JNIA vina madeni makubwa kutoka kwa
wapangaji wake ambao ni wafanyabiashara wakiwemo mawakala wa mashirika
ya ndege na mawakala wa kampuni za ndani na nje ya nchi.
"Wafanyabiashara
hawa kwa maslahi ya watu wachache wasio na uzalendo, tunafahamu kuwa
wanafatwa na kuombwa fedha kidogo ili deni kuu lisogezwe mbele ndio
sababu mpaka leo kuna baadhi wanadaiwa kodi mpaka ya miaka mitatu au
minne iliyopita.
"Sasa
nasema leo tutahitaji fedha yetu, mpaka Septemba 30 mwaka huu, hujalipa
deni la pango tunakuondoa anapewa mwingine tena kwa utaratibu mzuri tu
wa kutangaza na kushindanisha, " alisisitiza Waziri Mbarawa.
Vilevile
alisema lengo la maagizo hayo si kuwafukuza bali ni kufanya serikali
ifaidike na uwekezaji wake na wafanyabiashara wafurahie huduma bora
jambo litakalofanya viwanja vya ndege nchini viwe kibiashara badala ya
kuwa kama ofisi ya kawaida ya serikali kama inavyo sasa.
Alitumia
fursa hiyo pia kusikiliza kero mbalimbali za wafanyabiashara hao ambao
walisema wako tayari kulipa kodi zote na tozo kama inavyoagiza serikali
endapo huduma zitaboreshwa zaidi.
Huduma
walizozizungumzia ni pamoja na usalama, usafi hasa wa vyoo, uwepo wa
madaktari wa dharura kwa muda wote, uharaka wa upatikanaji wa visa kwa
abiria wanaowasili kiwanjani hapo na kutafuta suluhisho la muda mfupi la
mlundikano wa ndege kwenye maegesho.
Walisema
kwa nyakati tofauti kwamba sehemu ya maegesho ya ndege imekuwa ndogo
sana na kwamba inaleta usumbufu kwa marubani wanapotaka kuegesha ndege
zao baada ya kutua.
Aidha
walisema maofisa uhamiaji kiwanjani hapi ni wachache hivyo kusababisha
abiria kukwazika wanapowasili na kupoteza saa zima kusubiri huduma ya
visa tofauti na ilivyo kwenye viwanja vingine vya kimataifa.
Wafanyabiashara
hao pia walitumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mbarawa wafikiriwe kwa
kupewa kipaumbele kwenye nafasi za biashara mara jengo la Terminal III
litakapokamilika ujenzi wake.
Masuala
hayo yote Waziri Mbarawa aliyatolea ufafanuzi ambao uliwaridhisha
wafanyabiashara hao waliopongeza jitihada zake kwa kuwajali na kuandika
historia ya kufika na kuzungumza nao tangu waanze biashara kiwanja hapo.
Akihitimisha
ziara yake, Waziri Mbarawa aliwaagiza viongozi wa Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege (TAA) chini ya usimamizi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Salim
Msangi na Mamlaka ya Huduma za Uongozaji wa Ndege (TCAA) inayoongozwa na
Hamza Johari kukutana mara kwa mara na wateja wao ili kutatua
changamoto mbalimbali.
0 comments: