Advertisement |
Ijumaa, Agosti 25, mwaka huu, Kamati ya Ardhi na Mawasiliano wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar ilitembelea Makao Makuu ya Ofisi za Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA), yaliyopo jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam ili kuona na kupata taarifa mbali mbali zinazofanywa na
taasisi hiyo.
Taarifa
ya utendaji ya TMA iliwasilishwa na Selemani Selemani (Mchumi), ambaye pamoja na
mambo mengine, aliwafahamisha wajumbe wa kamati hiyo kuwa Mamlaka imepokea
‘Certificate of Appreciation’ toka Idara ya Kamisheni ya Kukaliana na Maafa na Mamlaka ya Usafiri
wa Majini (ZMA), kwa kazi nzuri inayofanywa ya kutoa huduma za hali ya hewa
katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Akizungumza
kwa niaba ya wajumbe, Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Ardhi na Mawasiliano wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma, alisifu kazi nzuri inayofanywa
na mamlaka katika kutoa huduma za hali ya hewa Zanzibar.
Mhe. Hamza aliielezea menejiment
ya TMA kuwa, huduma za hali ya hewa nchini zinazidi kuimarika hususan kwenye
usahihi wa taarifa zinazotolewa kama vile utabiri wa kila siku na tahadhari,
hivyo kuongeza imani kwa wananchi katika ufuatiliaji wa taarifa za hali ya hewa
ukilinganisha na hapo awali ambapo jamii
ilikuwa na hulka ya kupuuzia taarifa hizo.
Mjumbe mwingine aliyejitambulisha kwa jinala Mhe. Juma, alisema mchango wa TMA unatambuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ) akitolea mfano wa pongezi zilizotolewa kwa Mamlaka na Makamu wa Pili wa
Rais Mhe. Balozi Seif Ali Iddi kwenye Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
Kwa
upande wa TMA, Mwenyekii wa Bodi ya Ushauri Dk. Buruhani Nyenzi,
aliwashukuru wajumbe hao kwa pongezi zilizotolewa na kuahidi kuisaidia Mamlaka
kufikia malengo ya juu zaidi katika utoaji huduma kwa kuboresha miundo mbinu.
Aidha, aliwaeleza wajumbe hivi karibuni alikuwa na ziara ya kutembelea vituo vya
hali ya hewa vya Unguja na Pemba ili kujionea hali halisi, hivyo wananchi
wategemee huduma bora zaidi kwa kuwa lengo la Mamlaka ni kuongeza na
kuviboresha vituo vyake na kuongeza usahihi wa takwimu za hali ya hewa
zinazokusanywa.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, aliwashukuru wajumbe na kueleza
utendaji kazi wa Mamlaka kwa kuzingatia weledi na ushirikiano uliopo baina ya
wafanyakazi wenyewe na wadau wa hali ya hewa.
Alienda mbali zaidi na kusema anajivunia
uwepo wa wataalamu wa sayansi ya hali ya hewa wenye sifa za kitaifa na kimataifa
ambao mchango wao mkubwa umeonekana katika kuongeza usahihi wa taarifa
zitolewazo na TMA katika miaka kadhaa sasa mfululizo.
IMETOLEWA NA MONICA MUTONI, AFISA
HABARI WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.
0 comments: