Thursday, August 24, 2017

TTCL wapewa rai kuwafikia wa vijijini

ad300
Advertisement
Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), imeshauriwa kujizatiti kwenye kutanua upatikanaji wake maeneo ya vijijini ili Wananchi wa maeneo hayo wapate Mawasiliano ya uhakika kutoka katika Kampuni yao Umma.

Rai hiyo imetolewa na
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, alipozuru Makao Makuu ya TTCL ambapo alipata fursa ya kuzungumza na Bodi na Menejimenti ya TTCL.


Mhandisi Ngonyani amesema pamoja na mafanikio makubwa ambayo TTCL imeyapata katika Viwango vya ubora wa huduma, kuongeza idadi ya Wateja, usimamizi na uendeshaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Kutunzia Kumbukumbu za Kimtandao (NIDC) bado TTCL inakabiliwa na changamoto kubwa ya kufikisha huduma ya Mawasiliano Vijini hasa katika maeneo ambayo kwa sasa hayana Mawasiliano kabisa baada ya kuzimwa mwa mitambo ya Mawasiliano iliyokuwa ikitumia teknolojia ya CDMA.

Aidha, Mhe Ngonyani ameiagiza Bodi na Menejimenti ya TTCL kuongeza kasi ya kusambaza huduma za TTCL 4G pamoja na kufanyia kazi kilio cha muda mrefu cha Watumishi wa TTCL kuomba kuboreshewa Maslahi yao.

“Pote nilipopita Bara na Visiwani, Watumishi wa TTCL wameniomba nifikishe kilio chao kwenu, wamekaa kipindi kirefu sana bila kuboreshewa maslahi yao huku gharama za maisha zikiwa juu. Ninashauri msikie kilio hiki ili pamoja na kuboresha huduma zenu, mazingira ya kazi na maslahi ya Watumishi pia yapewe kipaumbele,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Mhandisi Omari Rashid Nundu amesema, Bodi na Menejimenti ya TTCL zimepokea maelekezo ya Naibu Waziri na kwamba mpango mkakati wa muda mfupi uliowekwa na Kampuni hiyo, changamoto hizo zitafanyiwa kazi.

“Mheshimiwa tunayo nia ya dhati ya kuibadilisha TTCL na kuifanya iwe kweli Kampuni ya Umma inayowaunganisha Watanzania. Tumedhamiria kuwafikia Wananchi wote kwa huduma za kiwango cha juu na unafuu sana wa gharama sambamba na kuimarisha vitendea kazi na maslahi ya Watumishi. Tunaomba Serikali iendelee kutuunga mkono na kutuwezesha kutimiza mipango hii,” alisema. 


Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema, TTCL mpya imejipanga kikamilifu kujiendesha kibishara na kufikia lengo la kutoa gawio Serikalini.

Aliongeza kuwa, TTCL kupitia kauli mbiu yake ya Rudi Nyumbani imekusudia kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata huduma za Mawasiliano kwa Teknolojia za 2G/3G na 4G LTE sambamba na huduma za kifedha za TTCL PESA ambayo imezinduliwa hivi karibuni.

Mapema mwezi ulipita, TTCL ilizindua huduma za kifedha kwa njia ya Mtandao ijulikanayo kama TTCL PESA ambapo pamoja na mambo mengine itawawezesha Wananchi kupata huduma mbali mbali kama Kutuma Fedha, Kulipia Ankara za huduma kama vile Maji, Umeme (LUKU), Ving’amuzi na Kununua vifurushi vya TTCL huku huduma nyingine zikiendelea kuongezwa.

TTCL PESA imeelezwa itasaidia katika kufanya makusanyo ya tozo za Serikali pamoja na kuongeza usalama na kupunguza hatari ya kupotea kwa fedha kupitia vitendo vya uhalifu kama ujambazi wanavyofanyiwa Wananchi (Wakulima na Wafugaji) wanaotembea na fedha nyingi katika maeneo mbali mbali wanapofanya biashara zao za mazao na mifugo.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: