Thursday, August 17, 2017

Sanduku la kura laokotwa shambani Kenya

ad300
Advertisement
Kasoro za Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 8, mwaka huu, zinadaiwa kuanza kujitokeza baada ya wafugaji katika Kaunti ya Turkana kuokoa sanduku la kura za Ugavana.

Sanduku hilo lililopatikana karibu na makutano ya Napeililim katika barabara ya Lodwar kwenda Kakuma, inadaiwa lilikuwa limefungwa lakini lilikuwa limetobolewa kwa chini.

Maofisa wa Chama cha Jubilee waliokuwa wa kwanza kuwasili eneo hilo baada ya kutaarifiwa na wafugaji walithibitisha kuwa sanduku hilo halikuwa na karatasi za kura ndani.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama hicho katika kaunti hiyo, James Kuya, alisema tundu lililoko kwenye sanduku hilo ni kubwa, ishara kwamba karatasi za kura zilizokuwemo zilitolewa.

“Masanduku yote ya uchaguzi na vifaa vingine vilivyotumiwa ni lazima viwe mikononi mwa serikali. Kwa nini sanduku hili liko hapa siku saba baada ya uchaguzi?” alihoji.

Alisema viongozi wa Jubilee katika kaunti hiyo walikuwa wamelalamika kuhusu jinsi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilivyosimamia uchaguzi eneo hilo.

Kufuatia tukio hilo, aliyekuwa mgombeaji ugavana wa chama cha Jubilee katika kaunti hiyo, John Munyes, amepanga kupinga ushindi wa Gavana Josphat Nanok wa Chama cha ODM.

Aidha katika hatua nyingine, Kiongozi wa NASA, Raila Odinga, ameendelea kulalamika kuwa yeye ndiye mshindi wa kiti cha urais kwenye uchaguzi wa Agosti 8, mwaka huu.

Kwenye moja ya mikutano yake baada ya kusema atakwenda mahakamani kudai haki yake, alidai aliyekuwa Meneja wa TEHAMA  wa IEBC, Chris Msando alitolewa kafara, ili Jubilee iwe na uwezo wa kuiba kura.

Akiwahutubia wafuasi wake kuhusu matokeo ya uchaguzi wa wiki iliyopita, Odinga alisema: "Tunamkumbuka kijana mdogo kwa jina Chris Msando ambaye alitolewa kafara na watu waliotaka kubaki madarakani.”

Kiongozi huyo wa muungano wa NASA alisema Wakenya hawatakubali viongozi walioshinda uchaguzi kwa kuvuruga mitambo ya IEBC akiwataja kuwa ni 'vifaraga wa kompyuta.'

Odinga aliendelea kusema alipotembelea familia ya marehemu Msando katika Mtaa wa Nyayo, Embakasi, jijini Nairobi, aliwaeleza juu ya masikitiko yake kwamba serikali ilikataa msaada wa Marekani na Uingereza katika uchunguzi wa mauaji hayo.

“Hatuna shaka katika akili zetu kuwa mauaji haya yalitekelezwa na watu ambao walitaka kuingilia uchaguzi mkuu uliopita. Serikali za Marekani na Uingereza ziliahidi kusaidia uchunguzi lakini mpaka sasa serikali imekaa kimya.

"Serikali haiwezi kufanya uchunguzi wa haki kwa sababu ndiyo mshukiwa wa kwanza lakini sisi tunataka mauaji ya Msando yachunguzwe kikamilifu,” alisisitiza.

Msando aliyeuawa Julai 31, wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu ambao alitarajiwa kutekeleza jukumu muhimu kuzuia wizi wa kura, atazikwa Jumamosi ijayo katika Kaunti ya Siaya.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: