Advertisement |
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB), ameshiriki Mkutano wa 47 wa maandalizi ya mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa msimu wa mvua za vuli (Oktoba-Desemba 2017) kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum-GHACOF-47).
Mkutano huo ulifanyika Zanzibar Beach Resort, Agosti 21-22, ambapo katika hotuba yake ya ufunguzi aliwapongeza wajumbe na washiriki mbalimbali wa mkutano huo kwa kuitumia sayansi waliyonayo kwa manufaa ya umma.
“Napenda kuwapongeza GHACOF kwa kuwezesha sayansi
ya hali ya hewa kutumika katika shughuli za maendeleo ya jamii, nikiangalia kwa
upande wa nchi yetu ya Tanzania kumekuwa na ongezeko la mahitaji na matumizi ya
huduma za hali ya hewa kwa kiasi kikubwa sambamba na wigo mpana wa uelewa wa
matumizi ya taarifa hizo ambazo zitasaidia sana wananchi kukabiliana na
mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema.
Aidha aliongezea kuwa baada ya taarifa hiyo kutolewa kila nchi shiriki ikiwemo Tanzania itakaa na kuandaa taarifa yake ambapo kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) taarifa rasmi itatolewa kwa vyombo vya habari tarehe 31 Agosti 2017.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Kituo cha Ufuatiliaji
wa Hali ya Hewa cha Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (ICPAC) Dk. Guleid
Artan akizungumza katika ufunguzi huo alisema, ICPAC kwa kushirikiana na
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wanatekeleza programu ya utoaji
wa tahadhari na kwa wakati (Integrated Regional Early Warning
System (IREWS)).
Alisema Program hiyo ina
lengo la kuhakikisha nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika wananufaika
kwa kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zitolewazo zinafika kwa jamii kwa
wakati na zinatumika katika kupunguza madhara ya yatokanayo na hali mbaya ya
hewa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Zanzibar Mhe.
Mwinyi Ussi Abdallah Hassan akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa
wa Mjini Magharibi aliwataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa kwa
karibu kwa kutumia njia za kisasa zilizopo.
GHACOF ni Mkutano unaowakutanisha
wataalamu wa hali ya hewa kama watoa huduma pamoja na wataalamu kutoka katika sekta
mbalimbali kama watumiaji kutoka nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika
kwa lengo la kujadili, kuandaa na kutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu
husika katika ukanda huu.
IMETOLEWA
NA: MONICA MUTONI, AFISA HABARI, MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
0 comments: