Advertisement |
Kampuni za
Independent Power Tanzania (IPTL) na Pan African Power Solutions
(T) Limited (PAP), zimewasilisha maombi mahakamani kutaka kampuni za
Standard Chartered Bank Hong Kong Limited na Standard Chartered Bank Malaysia
Berhard ziamriwe kuweka dhamana ya sh. bilioni 50.
IPTL na PAP
zimewasilisha maombi hayo wiki iliyopita, katika Mahakama Kuu, Kitengo cha
Biashara ambayo yanaungwa mkono na hati ya kiapo cha Wakili wao, Joseph
Makandege.
Katika maombi hayo
namba 241 ya mwaka huu, IPTL na PAP wanaiomba mahakama hiyo, kuziamuru benki
hizo kuweka dhamana ya sh. bilioni 50 kabla ya kusikiliza shauri
lililofungiliwa kupinga kusajiri hukumu ya Uingereza ambayo inazitaka kampuni
hizo kulipa benki hizo malipo ya Dola za Marekani 168,800,063 (zaidi ya sh. bilioni
376).
Maombi hayo
yamepangwa kusikilizwa Oktoba 10, mwaka huu, mbele ya Jaji Barke Sahel,
ambaye anasikiliza shauri la kupinga kusajiriwa kwa hukumu hiyo iliyotolewa na
Mahakama Kuu ya Biashara ya Uingereza.
Kupitia hati yake ya
kiapo, Makandege anadai benki hizo mbili ni mali za kigeni na zimesajiliwa
nchini China na Malaysia. Pia anadai benki hiyo hazina mali yoyote Tanzania inayoweza
kufidia gharama zitakazotumiwa na kampuni hizo kuendesha shauri hilo hapa
nchini.
Aidha, anadai wakili
anayeziwakilisha benki hizo ameshindwa kuonyesha mahakamani au kwa wateja wake
uhalali wa kuendelea kusimamia shauri hilo au kufungua mashauri yoyote kwa
niaba ya benki hizo.
Makandege anadai
hakuna maofisa wa juu wa benki hizo waliotia saini nyaraka au kumbukumbu
zilizowasilishwa mahakama kupinga shauri hilo, hivyo itakuwa vigumu kwa IPTL na
PAP kuwataka maofisa hao kuwajibika kwa kile kitakachotokea baadae.
“Hata nchi kule ambazo
benki hizo zilikotoka hazina mikataba au utaratibu na Tanzania wa kutekeleza
hukumu zinazotolewa na mahakama za nchi hizo hapa nchini, kitendo ambacho kinaweza kuzihakikishia IPTL na PAP kulipwa
gharama watakazozitumia baada ya shauri hilo kufika mwisho.
Katika hati yake ya
kiapo, Makandege anafafanua kiwango cha fedha kinachodaiwa na benki hizo dhidi
ya wateja wake (IPTL na PAP) ambacho ni Dola
za Kimarekani 168, 800,063 (sawa na sh. 376,424,142,274), ni kikubwa ambapo inahitajika
gharama kubwa na haijaonyeshwa kama wateja wake wamesamehewa kulipa gharama ya
kujitetea.
Anadai benki hizo
zimekuwa na mwenendo wa kubadili misimamo na wakati mwingine kuondoa au kufuta
mashauri waliyoyafungua mahakamani, jambo ambalo limekuwa likiwasababishia
walalamikiwa kuingia gharama kubwa za
kujitetea bila msingi wowote.
Wakili huyo anadai hukumu ya nje inayotaka kusajiriwa imeghubikwa
na makosa mengi, jambo ambalo linasababisha kuwepo na uwezekano mkubwa wa
kutokubaliwa na mahakama za hapa nchini.
Makandege anadai
wakati IPTL, PAP na VIP Engineering and
Marketing Limited zilipokuwa zinapambana Uingereza ziliamriwa kuweka dhamana
kwa ajili ya gharama za benki hizo kujitetea kwa kuwa kampuni hizo hazisajiriwa
huko na wala hazina mali yoyote
inayoweza kufidia gharama hizo.
Katika shauri la
msingi, IPTL na PAP wanaiomba mahakama hiyo kutengua amri iliyotolewa Februari
9, mwaka huu, kusajiri hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Malkia Uingereza, Idara ya
Mahakama ya Biashara ya Novemba 16, mwaka jana kuhusu malipo hayo.
IPTL na PAP wanaiomba
mahakama itamke hukumu ya kigeni iliyosajiliwa mbele ya Jaji Sahel haisajiliki
na wala haitekelezeki nchini Tanzania.
0 comments: