Friday, August 18, 2017

Alichokisema mchumi wa BoT kuhusu uchumi wa Tanzania

ad300
Advertisement
Lusajo Mwankemwa

Mchumi
Kurugenzi ya Sera za Uchumi na Utafiti
Benki Kuu ya Tanzania (BoT)

VIASHIRIA VYA UKUAJI WA UCHUMI NA MWENENDO
WA HALI YA UCHUMI  WA TAIFA KWA MWAKA 2016

Ukuaji wa Pato la Taifa

"Ukuaji wa uchumi ni mojawapo ya viashiria vinavyotazamwa katika kutathmini afya ya uchumi wa Taifa. Ukuaji wa uchumi unapimwa kwa kutumia ukuaji wa Pato la Taifa yaani thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa katika nchi katika kipindi kinachorejewa ikilinganishwa na kipindi kilichopita. Takwimu za ukuaji wa Pato la Taifa zinaonesha kuwa uchumi wa Taifa umeendelea kukua na Tanzania imebaki kuwa miongoni mwa nchi za bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa zaidi. Mifano ya nchi jirani kama ifuatavyo.

Jedwali1: Ukuaji wa Pato la Taifa Katika Baadhi ya Nchi za Kiafrika
NCHI
2015
2016 (Matarajio)
Burundi
-4.0
-0.5
Kenya
5.6
6.0
Rwanda
6.9
6.0
Tanzania
7.0
7.0 (halisi)
Uganda
4.8
4.9
Zambia
3.0
3.0
Malawi
2.9
2.7
Congo DRC
6.9
3.9
Afrika Kusini mwa Sahara
3.4
1.4


Katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2016 kiwango halisi cha ukuaji wa Pato la Taifa kiliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 6.5 ikilinganishwa na kiwango cha ukuaji cha asilimia 6.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Kwa ujumla, sekta nyingi zilikua kwa kasi isipokuwa sekta chache. Sekta zifuatazo zilikuwa na viwango vikubwa vya ukuaji katika kipindi hicho: shughuli za uchimbaji madini na mawe (asilimia 15.8); shughuli za usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (asilimia 15.5); habari na mawasiliano (asilimia 13.4); na huduma za fedha (asilimia 11.5).

Maoteo ya ukuaji wa Pato la Taifa kwa mwaka 2016 (Januari-Desemba) yalitarajiwa kuwa asilimia 7.2. Hata hivyo ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2016 ulifikia asilimia 7.0, chini ya matarajio, hali ambayo ilitokana na mwenendo wa uchumi katika miezi tisa ya mwanzo ambapo sekta zinazoajiri watu wengi na zenye mchango mkubwa katika uchumi hazikukua katika kasi iliyotarajiwa ikiwemo sekta ya kilimo ambayo ilikua kwa wastani wa asilimia 2.1 (matarajio ya mwaka ni asilimia 2.6) na biashara ilikua kwa wastani wa asilimia 5.6 (matarajio ya mwaka ni asilimia 7.6).  Aidha, kuzorota  kwa uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Ulaya na China ambao ni wabia wetu wakubwa wa biashara na uwekezaji ndio kumechangia kupunguza matarajio ya awali ya kasi ya ukuaji  wa uchumi nchini. Kasi ya ukuaji wa uchumi wa China inakadiriwa kupungua kutoka asilimia 6.9 mwaka 2015 hadi asilimia 6.6 mwaka 2016.

Mfumuko wa bei

Kiashiria kingine cha jumla cha afya ya uchumi wa Taifa ni mfumuko wa bei ambao unapima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini. Mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia 6.5 Januari 2016 hadi asilimia 5.5 Juni 2016 na kupungua zaidi hadi asilimia 4.5 Septemba 2016 na baadaye kupanda kidogo mwezi Desemba na kufikia asilimia 5.0. Aidha, mfumuko wa bei kwa mwaka mzima wa 2016 ulipungua na kufikia wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2015. Maana yake ni kuwa bei za bidhaa na huduma ziliongezeka kwa kasi ndogo zaidi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma. Mwenendo huu wa kushuka mfumuko wa bei ulichangiwa na kasi ndogo ya ongezeko la bei za chakula nchini, kushuka kwa wastani wa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia, utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti na fedha, na utulivu wa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya kimarekani.

Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubakia katika viwango vya tarakimu moja katika siku zijazo na kubakia ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5.0. Matarajio haya yatategemea kuendelea kutulia kwa bei ya nishati nchini kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa umeme, mwendelezo wa sera thabiti ya fedha na kibajeti, kutobadilika sana kwa bei za mafuta katika soko la dunia, pamoja na kuendelea kuwepo kwa utulivu wa thamani ya Shilingi. Hata hivyo, kuna viashiria vinavyoonesha uwezekano wa kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutokana na hali ya ukame uliojitokeza hapa Tanzania na kwa baadhi ya nchi za ukanda wa nchi za Afrika Mashariki pamoja na uwezekano wa kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia.





Mfumuko wa bei katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

1.        Wastani wa mfumuko wa bei kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliendelea kuwa imara na kubakia katika wigo wa tarakimu moja mwaka 2016. Nchini Kenya, mfumuko wa bei ulipungua kufikia wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2016 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.6 mwaka 2015. Hata hivyo, mfumuko wa bei nchini Uganda ulipanda na kuwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.2 mwaka 2015.

Thamani ya shilingi

2.        Kiashiria kingine cha afya ya uchumi ni uimara wa thamani ya shilingi. Katika kipindi cha Julai – Desemba 2016, Serikali iliendelea na utekelezaji wa sera za fedha na bajeti, hatua zilizowezesha kuimarika kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani. Katika kipindi hicho, thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani ilipungua kwa kasi ndogo kutoka wastani wa shilingi 2,144.27 kwa dola moja mwezi Desemba 2015 hadi shilingi 2,170.44 kwa dola moja mwezi Desemba 2016. Kuimarika kwa thamani ya shilingi kulitokana na hatua mbalimbali za sera ya fedha zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kusimamia hali ya ukwasi kwenye uchumi pamoja na kuimarika kwa urari wa bidhaa na huduma katika sekta ya nje.  Aidha, thamani ya Shilingi kwa Dola ya Kimarekani ilishuka (kwa takriban asilimia 2.15 katika kipindi cha miezi kumi na mbili kufikia tarehe 19 Januari 2017), kufuatia kuimarika kwa Dola ya Kimarekani. Kuimarika kwa Dola ya Kimarekani kuliathiri pia sarafu nyingine zikiwemo yuan ya China (iliyoshuka thamani kwa asilimia 3.55 katika kipindi cha miezi kumi na mbili kufikia tarehe 19 Januari 2017), shilingi ya Uganda (asilimia 3.7), Faranga ya Rwanda (asilimia 8.55), na Pauni ya Uingereza (iliyoshuka thamani kwa asilimia 13.04).

3.        Kuimarika kwa Dola ya Kimarekani kulitokana zaidi na kupanda kwa riba ya sera ya fedha (policy rate/Fed Fund rate) mwezi Desemba 2016, hali iliyosababisha wawekezaji kuongeza mahitaji yao ya Dola ya Kimarekani kwa ajili ya kuwekeza. Aidha, kwa upande wa Tanzania mwezi Januari ni msimu wa mapato madogo ya fedha za kigeni zitokanazo na mauzo ya mazao ya biashara, hali ambayo imechangia pia kuwa na dola pungufu kwenye soko la fedha.

Sekta ya Nje na Akiba ya Fedha za Kigeni

4.        Katika mwaka 2016, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia 48.8 na kufikia nakisi ya Dola za Kimarekani milioni 2,054.8, kutoka nakisi ya Dola za Kimarekani milioni 4,011.6 kwa mwaka 2015. Kupungua huko kulitokana zaidi na ongezeko la thamani ya madini hususan dhahabu, bidhaa asilia, mapato yatokanayo na utalii, pamoja na kupungua kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za kukuza mitaji, na bidhaa za matumizi ya kawaida. Katika kipindi hicho, thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 5.2 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 9,381.6 wakati thamani ya bidhaa na huduma toka nje zilipungua kwa asilimia 13.7 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 10,797.4

5.        Hadi mwezi Desemba 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola ya Kimarekani milioni 4,325.6 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4.2. Aidha, rasilimali za fedha za kigeni za mabenki ya biashara zilifikia Dola ya Kimarekani milioni 768.2, wakati amana za fedha za kigeni zilizohifadhiwa na wakazi katika benki za biashara zilifikia Dola za Kimarekani milioni 2,870.8. Hivyo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha.


Hali ya Ukwasi katika uchumi

6.        Ukwasi (liqudity) ni kiasi cha fedha kilichopo katika uchumi na unajumuisha fedha taslim, amana katika mabenki zilizopo Benki Kuu. Utoshelevu wa ukwasi katika uchumi unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali ikiwemo ujazi wa fedha, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi, kiwango cha mitaji ya mabenki, uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi, na upatikanaji wa huduma za kifedha. Pale ambapo imedhihirika kuwa kuna upungufu wa ukwasi katika uchumi, Serikali kupitia Benki Kuu huchukua hatua mbalimbali za kisera kuchochea shughuli za kiuchumi. Hatua hizi ni pamoja na kuongeza ujazi wa fedha na kuboresha mazingira kwa sekta binafsi kukopa. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inaweza kupunguza kodi na kuongeza matumizi ya Serikali.


Hali ilivyo sasa

7.        Hali ya baadhi ya vigezo vya ukwasi nchini ni kama ifuatavyo: kwa kutumia kigezo cha uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika kwa muda mfupi (Liquid assets to Demand Liabilities), uwiano huu ulikuwa asilimia 42.4 ukilinganishwa na asilimia 37.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2015 na ikilinganishwa na uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20. Amana za wateja katika mabenki zilipungua kidogo kutoka shilingi trilioni 20.73 mwezi Desemba 2015 kufikia shilingi trilioni 20.57 mwezi Septemba 2016. Miongoni mwa sababu zilizochangia kupungua kwa amana kwenye mabenki ni pamoja na uamuzi wa Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya umma kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo, amana za serikali kwenye mabenki ya biashara ni asilimia 3 tu ya amana zote za mabenki.  Aidha, jumla ya rasilimali za mabenki zimeendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 26,917.2 mwezi Desemba 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 27,978.2 mwezi Desemba 2016, sawa na ongezeko la asilimia 2.6.

Mikopo kwa Sekta Binafsi

8.        Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 7.2 katika kipindi cha mwaka ulioishia Desemba 2016 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 24.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji kulitokana na tahadhari iliyochukuliwa na mabenki kufuatia kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 6.4 Desemba, 2015 hadi asilimia 9.5 Desemba, 2016.

9.        Ni vema pia ieleweke kuwa kupungua kwa kasi ya kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi katika miezi ya hivi karibuni siyo kwa Tanzania pekee. Kwa mfano, kiwango cha ukuaji wa mikopo kwenda sekta binafsi katika nchi jirani ya Kenya kilipungua kutoka asilimia 19.7 kati ya Julai na Oktoba 2015 hadi kufikia asilimia 4.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Aidha, Nchini Uganda mikopo kwa sekta binafsi ilipungua kutoka asilimia 25.2 mwezi Septemba 2015 hadi asilimia -1 mwezi Septemba 2016. Pia mwenendo usioridhisha ulijitokeza katika mikopo chechefu katika nchi hizo jirani na kusababisha baadhi ya mabenki hususan Crane Bank ya Uganda kuwekwa chini ya uangalizi. Hali ni mbaya zaidi kwa nchi kama Nigeria na Ghana zinazouza mafuta.

Uamuzi wa Serikali Kuzitaka Taasisi za Umma Kufungua Akaunti za Mapato Benki Kuu kama sababu ya Kupungua kwa Ukwasi katika uchumi.

10.     Ni vyema jamii ya Watanzania ikafahamu kwamba akaunti ambazo fedha za mashirika zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za kukusanya mapato tu na amana za muda maalum. Akaunti za matumizi bado ziko katika benki za biashara ili kuyawezesha mashirika kufanya malipo kupitia akaunti hizo. Hivyo, bado benki za biashara ni kiungo muhimu kati ya mashirika ya umma na watoa huduma kwa mashirika hayo. Hatua iliyochukuliwa na Serikali inalenga kuzisukuma benki za biashara kuchukua hatua za ziada kupanua huduma za kifedha hadi vijijini badala ya kujikita mijini zaidi kuhudumia makampuni makubwa (corporate sector) na kufanya biashara katika soko la dhamana na hati fungani za Serikali. Uamuzi huu umesaidia katika usimamizi wa mapato na matumizi ya Mashirika hayo na pia kurahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha kupitia Benki Kuu. Aidha, Serikali imeacha kukopa fedha zake yenyewe na kwa gharama kubwa. Kwa kuwa amana za Serikali kwenye mabenki ya biashara ni sehemu ndogo tu (asilimia 3) ya amana zote za mabenki, madai kwamba uamuzi wa Serikali kuondoa fedha za mashirika na taasisi kwenda kwenye akaunti za mapato BOT umesababisha kupungua kwa ukwasi hayana uzito.

Mwenendo wa Deni la Taifa

11.     Deni la Taifa linajumuisha mikopo ambayo hukopwa na Serikali kutoka nje na ndani ya nchi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kujaza nakisi ya bajeti. Deni la nje hukopwa kutoka kwenye taasisi za kifedha kama vile Benki ya Dunia, nchi Wahisani na pia kutoka kwenye benki za biashara wakati deni la ndani linapatikana kwa kuuzwa kwa dhamana za Serikali (treasury bills) na hatifungani (Treasury bonds), mikopo kutoka Benki Kuu ya Tanzania na benki za biashara za ndani.

12.     Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134.  Aidha, katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linasimamiwa kikamilifu Serikali inakamilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 ili kuimarisha usimamizi wa Deni la Taifa.

13.     Hadi kufikia Desemba, 2016, Deni la Taifa likijumuisha deni la ndani na la nje lilifikia Dola za Kimarekani milioni 19,021.9 (debt stock) ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 18,459.3 Juni, 2016 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 3.05. Kiasi hiki cha deni hakijumuishi deni la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii linalokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni 1,725.8 ingawaje deni hilo limezingatiwa katika tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa.

14.     Ongezeko la deni hilo limetokana  na mikopo iliyopo na mipya iliyopokelewa na Serikali na ambayo bado haijaiva kutoka mikopo ya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile reli ya Tazara, daraja la Kikwete mto - Malagarasi, barabara ya Morogoro – Dodoma, barabara ya Dodoma – Singida – Arusha, barabara ya Mwanza – Bukoba, mradi wa Maji ziwa Victoria, Bomba la Gesi Mtwara – Dar es Salaam, barabara ya Dodoma - Singida – Mwanza, miradi ya umeme Kinyerezi I & II, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano n.k.




Ulipaji wa Deni la Taifa

15.     Ulipaji wa Deni la Taifa hauangalii ukubwa wa deni lililopo (stock of debt) bali kadri deni linavyoiva (debt maturity). Hali ilivyo sasa sehemu kubwa ya Deni la Taifa linaiva kwa kipindi cha muda mrefu (long term maturity). Kutokana na hali hiyo, kwa wastani (average time to maturity) wa deni lililopo sasa litaiva katika kipindi cha miaka isiyopungua 11.9. Hali hii inaashiria kwamba athari zake kwenye bajeti ziko chini (low refinance risk).

16.     Serikali imekuwa ikilipa madeni ya nje na ndani kwa mujibu wa mikataba. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia Desemba, 2016 Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 2,570.1 kulipia madeni ya ndani na nje yaliyoiva. Kati ya kiasi hicho, malipo ya deni la ndani ni shilingi bilioni 1,822.3 na deni la nje ni shilingi bilioni 747.8. Malipo ya deni la ndani yanajumuisha malipo ya mtaji (rollover) ya shilingi bilioni 1,367.1 na malipo ya riba ya shilingi bilioni 455.2

Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa
17.     Katika tathmini iliyofanyika Novemba 2016, viashiria vinaonesha kuwa: thamani ya sasa ya jumla ya deni la Taifa (Present Value of Total Public Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56, thamani ya sasa ya Deni la nje pekee (Present Value of External Debt)  kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya sasa ya  deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimi 250.

18.     Kutokana na tathimini,  ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 11.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20 na Ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Kwa kuzingatia vigezo hivyo, Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa toka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje kwa wakati.







Jedwali Na. 2: Viashiria vya Uhimilivu wa Deni Taifa
VIASHIRIA VYA DENI LA NJE
2015/16
2016/17
2017/18
2020/21
2025/26
2035/36
Ukomo
Deni la nje (PV ) /Pato la Taifa
19.9
19
18.8
20.1
18.9
14.2
40
Deni la nje  (PV) / uuzaji wa bidhaa nje
97.7
94.2
98.2
107.4
95.5
71.0
150
Deni deni la nje (PV) / Mapato ya ndani
145.3
111.46
114.3
98.7
91.8
68.39
250
Ulipaji wa deni la nje/Uuzaji wa bidhaa nje
7.8
9.2
8.4
8.0
7.9
8.0
20
Ulipaji wa deni/ Mapato ya ndani
11.5
11.0
9.7
7.3
7.6
7.7
20
VIASHIRIA VYA DENI LA NJE NA LA NDANI (Total Debt)


Deni (PV) /Pato la Taifa
34.2
32.5
31.2
32.7
29.4
23.3
56
Deni (PV) / Mapato ya ndani
30.8
21.1
23.4
16.9
16.6
16.1


19.     Kutokana na muundo wa deni la Tanzania (debt structure) sehemu kubwa ya madeni yake yanaiva kwa muda mrefu (miaka 5 hadi 50). Hivyo, upimaji wa deni la Taifa huangaliwa kwa kutumia thamani ya sasa ya deni (Present value of debt) badala ya kutumia thamani halisi ya deni (nominal value of debt) hii inaiwezesha tathmini iweze kufanyika kwa madeni yanayoiva kwa muda mrefu kinyume na thamani halisi ya deni kwa pato la Taifa (nominal value of debt to GDP), ambayo inaangalia hali ya deni kwa muda mfupi. Kwa kuzingatia hali hiyo, viashiria vilivyooneshwa hapo juu ndio viashiria sahihi vilivyokubalika kimataifa katika upimaji wa uhimilivu wa Deni la Taifa.

Kwa kuzingatia vigezo hivyo, uwiano wa deni lote la ndani na nje kwa thamani ya sasa kwa pato la Taifa (PV of total public debt/GDP) kwa mwaka 2015/16 Kenya ilikuwa asilimia 45.6, Tanzania asilimia 34.2, Uganda asilimia 24.1, na Rwanda asilimia 22.7.  Vile vile, uwiano wa deni la nje kwa thamani ya sasa kwa Pato la Taifa: Kenya ilikuwa asilimia 19.4; Tanzania asilimia 19.9; Uganda asilimia 10.7; Rwanda  asilimia 17.3 (PV of external debt/GDP) ambavyo vyote bado viko chini ya ukomo. 
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: