Wednesday, July 19, 2017

TTCL yazindua TTCL PESA, yaahidi kiwanda cha simu

ad300
Advertisement
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akiwa na CEO wa TTCL, Waziri Kindamba na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Omary Nundu mara baada ya uzinduzi wa huduma ya TTCL PESA, jijini Dar es Salaam.
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), imesema baada ya kuzindua huduma ya TTCL PESA, ipo kwenye maandalizi ya kuanzisha kiwanda cha simu za kisasa za mkononi 'Smartphone' kama moja ya mfululizo wa jitihada zake za kuiunga mkono serikali inayosisita uchumi wa viwanda.

Imesema mpango huo ni miongoni mwa iliyowekwa na uongozi mpya wa kampuni hiyo ukiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi, Menejimenti na watumishi wote wa kampuni hiyo kwa kipindi kifupi tangu kuanza kufanya kazi pamoja.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam Julai 18, na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alipozungumza kwenye hafla ya uzinduzi rasmi wa huduma za kifedha za kampuni ya simu ya TTCL (TTCL PESA), iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, makao makuu ya kampuni hiyo.

Alisema mazungumzo ya kuwepo kwa kiwanda hicho yameanza dhidi ya kampuni na mashirika mbalimbali lakini kabla ya hilo kutimia, wameleta TTCL PESA itakayotoa huduma za kifedha kwa wananchi kwa gharama nafuu ili kusukuma ajenda ya nchi ya uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Ofisa huyo huku akimkaribisha makamu wa rais kuzungumza na umma kwenye hafla hiyo, alisema huduma hiyo mpya, ya kihistoria ya TTCL itawawezesha wananchi kutuma fedha, kupokea, kulipia ankara mbalimbali ikiwemo kodi, umeme na maji kwa unafuu wa asilimia 10 mpaka 50 kulinganisha na kampuni zingine za simu hapa nchini.

"Kwa ujumla sasa TTCL ni mpya, inasikiliza maoni ya wananchi kupitia vituo vyetu vya huduma kwa wateja vilivyoboreshwa kwa mandhari ya kisasa na watendaji wenye weledi wa kutosha kuhudumia wateja kwa kasi na ufanisi," alisema.

Makamu wa Rais, yeye kwa upande wake pamoja na kuipongeza kampuni hiyo kwa mafanikio hayo, aliitaka itoe kipaumbele kwenye kuwapatia wanawake huduma nafuu za kifedha kwa kupitia mpango mpya wa TTCL PESA ili hatimaye wawe sehemu ya mchango kwenye ukuaji wa uchumi wa taifa.

Alisema licha ya kuwa wengi kwa asilimia takriban 51 kulingana na sensa ya mwaka 2012, wanawake wana changamoto ya kutofikiwa na huduma za kifedha na benki hivyo fedha zao nyingi hupotea mara kwa mara na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

"Mwanamke anaweza kupata fedha nyingi lakini hana akaunti benki, hivyo fedha zake hupotea tu kwa hiyo ninawasihi muwaangalie wanawake kwenye huduma hii mpya, wataibeba TTCL mkiwatumia vizuri," alisema makamu wa rais.

Pia alisema TTCL inatia matumaini kwa kasi iliyonayo sasa, baada ya kukumbwa na matatizo lukuki kwa miaka mingi iliyopita ikiwa chini ya ubia wa kampuni ya Bharti Airtel na serikali hivyo uongozi uliopo uendelee ili serikali ifikiria namna ya kuiwezesha zaidi kama ambavyo tayari imefanya.

"TTCL ilikuwa na hali mbaya, sote ni mashahidi kwa kuliona hili na kutambua umuhimu wake kiuchumi, tuliirudisha serikalini, tukaruhusu TTCL itumie rasilimali zake kama dhamana ili ikopesheke kwa ajili ya uwekezaji na kuipa masafa yaliyofanikisha kufungwa kwa teknolojia ya 2G, 3G na 4G.

"Si hivyo tu, serikali ilitoa dhamana kwa TTCL kusimamia na kuendesha mkongo wa taifa wa mawasiliano (NICTBB) na kituo mahiri cha kimataifa cha kutunzia kumbukumbu za mtandao lengo likiwa moja tu la kuifufua kampuni hii ili itoe ushindani kwenye sekta ya mawasiliano," alisema.

Makamu wa rais pia alitumia fursa hiyo kuutaka umma kutumia huduma za kampuni ya TTCL na TTCL PESA, kwa sababu kwa sasa zina ufanisi mkubwa hivyo mbali na kutumia mitandao mingine, waongeze uzio kwa kuhamia TTCL ambayo ni kampuni ya kizalendo ya mawasiliano ya simu.

Katika uzinduzi huo, ulioshuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Omary Nundu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Angelina Madette, aliahidi kuwa wizara yake itaendelea kuunga mkono jitihada za kampuni hiyo ya umma kusonga mbele na kuliletea taifa maendeleo ya kiuchumi.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: