Monday, July 24, 2017

Mwanzilishi wa sare za Magereza za sasa astaafu

ad300
Advertisement
Mwanamke wa kwanza kufikia cheo cha Naibu Kamishna wa Jeshi la Magereza Tanzania, Edith Mallya (Pichani), amestaafu rasmi utumishi wa umma na kuacha neno zito kwa jeshi hilo kuelekea uchumi wa viwanda.

Amesema jeshi hilo kwa sasa liko kwenye mikono salama mara mbili zaidi ya awali, ambapo aliwataka watendaji na askari wanaosalia kwenye utumishi kutanguliza uzalendo wakati huu ambao jeshi hilo linafanya jitihada za kufufua viwanda vyake na kuanzisha vipya.

"Magereza ya sasa si kama tuliyoanza nayo mwaka 1977 nilipoanza kazi, ina uongozi makini na serikali ya awamu ya tano imeonyesha kwa vitendo mategemeo yake kwa jeshi kuufikia uchumi wa viwanda hivyo lazima wanaobaki watambue taifa linawategemea," alisema.

Edith, ambaye mpaka anastaafu alikuwa Mkurugenzi wa Viwanda wa Jeshi la Magereza, mwishoni mwa wiki iliyopita aliagwa kwa gwaride rasmi la kijeshi pamoja na wenzake watatu katika hafla iliyofanyika Chuo cha Magereza Ukonga, Dar es Salaam.

Afande huyo mwenye historia kubwa kwenye jeshi hilo ikiwemo kubadilisha sare za wafungwa kutoka rangi nyeupe kwenda zinazotumika sasa pamoja na kushirikiana na watendaji wengine kubadili matumizi ya malori kusafirishia wafungwa, mahabusu kwenda mahakamani alisema anastaafu huku akiishukuru serikali ya Dk. John Magufuli kwa kumwamini.

"Najivunia kuwa mwanamke pekee kuwa naibu kamishna wa magereza, ni jukumu zito lakini nilifanikiwa kwa ushirikiano nilioonyeshwa na uongozi wa nchi na jeshi ujumla sitasahau mchango wao kwenye mafanikio niliyoyapata kwenye utumishi wangu," alisema.

Pia aliongeza kwa kusema kuwa anafarijika kuona anaondoka kwenye jeshi hilo huku akiliacha limesheheni vijana wengi, ambao bado wana damu inayochemka kulitumikia jeshi la magereza na taifa kwa ujumla kwa miaka mingi ijayo jambo ambalo ni hazina.

Kuhusu kipindi ambacho hatakisahau kwenye utumishi wake magereza, alisema ni wakati akiwa mkuu wa gereza la Maweni la mkoani Tanga, ambako alikuwa akitukanwa na wafungwa wanaosubiria kunyongwa kwa kigezo cha kuwa mwanamke huku kukiwa na migomo ya mara kwa mara ya wafungwa.

"Ulikuwa wakati mgumu sana kwangu lakini nilifanikiwa kuupita, nikaweza kudhibiti nidhamu ya wafungwa ambao walitusaidia kuanzisha mashamba makubwa ya uzalishaji kwenye wilaya zote za mkoa wa Tanga amabyo mpaka leo yanasaidia sana magereza yetu," alisema.

Maofisa wengine wa jeshi hilo kutoka makao makuu walioagwa juzi pamoja na Afande Mallya ni makamishna wasaidizi waandamizi Marcela Lori, George Kuria na kamishna msaidizi Erasmus Kundi.

Hivi karibuni, Rais Dk. John Magufuli aliteua makamishna wapya kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wastaafu wa jeshi hilo ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwavika vyeo vya kuwa Naibu Kamishna wa Magereza SACP Uwesu Ngarama; SACP Gideon Mkana (Mkuu wa Chuo cha TCTA); SACP Jeremiah Nkondo (RPO-Kagera); SACP Tusekile Mwaisabila (RPO-Lindi) na SACP Augustine Mboje (RPO-DSM).

Wengine 24 waliopandishwa vyeo kuwa Makamishna Waandamizi Wasaidizi wa Magereza (SACP) ni ACP Mbaraka Semwanza; ACP George Mwambashi; ACP Charles Novati; ACP Faustine M. Kasike; ACP Joel Bukuku; ACP Deogratius Lwanga; ACP Boyd Mwambingu (RPO Pwani); ACP Athumani Kitiku (RPO Mwanza) na ACP Hassan Mkwiche (RPO Kilimanjaro).

Aidha, walikuwemo pia ACP Luhende Makwaia; ACP Hamza Hamza; ACP Jeremiah Katengu; ACP Mzee Nyamka (Kaimu RPO Morogoro); ACP Afwilile Mwakijungu (Mkuu wa gereza la Isupilo, Iringa); ACP Ali Kaherewa (Kaimu RPO Singida); ACP Ismail Mlawa (RPO Mtwara); ACP Chacha Jackson; ACP Rajab Bakari; ACP Kijida Mwankingi; ACP Julius Ntambala; ACP Mussa Kiswaka; ACP Justin Kaziulaya na ACP Bertha J. Minde.

Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: