Advertisement |
Katika utabiri huo, TMA imeonyesha matarajio makubwa katika uwepo wa mvua nyingi zitakazokuwa na manufaa kwa shughuli za ukuzaji uchumi ikiwemo kilimo na uvuvi.
Pia imetoa tahadhari kuhusiana na masuala ya afya kutokana na kuwepo uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya milipuko kwenye baadhi ya maeneo, kutokana na kutuama kwa maji taka yatakayokuwa hayadhibitiwi na wananchi, sekta husika.
Akitangaza utabiri huo mbele ya waandishi wa habari mkoani Morogoro juzi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema mvua za vuli za msimu huu zitakuwa za wastani hadi juu ya wastani kwenye maeneo kadhaa nchini.
Alisema mvua za juu ya wastani ambazo zinaweza kusababisha madhara zinatarajiwa kunyesha kuanzia wiki ya pili ya mwezi huu kwenye baadhi ya maeneo ya kanda ya ziwa mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga.
Kwa ukanda wa pwani ya Kaskazini, Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba, Dk. Agnes alisema mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani ambapo amezitaka Mamlaka za miji kuifanyia kazi mifumo ya maji safi na taka ili kuepusha madhara makubwa yakiwemo mafuriko.
Pia Mkurugenzi huyo alisema mvua kwenye mikoa ya kaskazini ikiwemo Kilimanjaro, Arusha na Manyara pia zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani na kwamba zitaanza wiki ya pili hadi ya tatu ya mwezi huu.
Hatahivyo, Dk. Agnes alibainisha kuwa nchini kuna baadhi ya maeneo ambayo yanapata mvua katika msimu mmoja pekee kwa mwaka, hususan mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa ambapo mvua za vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Novemba zikiwa katika kipimo cha wastani hadi juu ya wastani.
Aidha katika maeneo ya kusini mwa nchi, mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombealisema utabiri ulionyesha kuwepo kwa mvua za wastani hadi juu ya wastani, ambazo zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Novemba huku mkoa wa Ruvuma ukitegemewa kupata mvua chini ya wastani kwa kipindi hiki.
Kwa hali hiyo Dk. Agnes alisema Wananchi wanatakiwa kuzingatia maeneo ya kuishi, kuepuka maeneo ya mabondeni, huku akiwataka wakulima kuzitumia vizuri mvua za msimu huu kutokana na uwepo wa unyevunyevu kwenye maeneo makubwa ya nchi kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha.
0 comments: