Advertisement |
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam na Kaimu katibu mtendaji wa tume hiyo, Profesa Magishi Mgasa, alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusiana na maamuzi yao juu ya chuo hicho kutokana na ukaguzi walioufanya kwenye vyuo vyote nchini.
Profesa Mgasa alisema pamoja na onyo hilo, TCU imesitisha udahili wa wanafunzi wapya waliokuwa wameomba kuendelea na elimu ya juu kwenye chuo hicho katika mwaka wa masomo 2014/15, hatua ambayo haiwadhuru wanafunzi ambao wanaendelea na masomo katika chuo hicho.
Alisema sababu kuu za kufanya hivyo ni kutokana na mfumo mbovu wa uongozi na utawala uliopo chuoni hapo, ambapo kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya viongozi wa juu kinyume na utaratibu, pamoja na kitendo cha kuanzisha programu ya ngazi ya cheti bila kibali kutoka Tume ya Vyuo Vikuu hivyo .
Pia alisema tatizo la ukosefu wa Wahadhiri walio na sifa za kufundisha, miundombinu mibovu ya kufundishia, na tabia ya chuo hicho kudahili wanafunzi bila kufuata taratibu zilizowekwa na TCU ni sababu zingine zilizokifanya chuo hicho kupewa onyo la kubadilika kiutendaji.
Aidha alisema kutokana na mapungufu hayo, Septemba 16 mwaka huu TCU walitoa notisi kwa IMTU ili waweze kuyafanyia marekebisho kwasababu tofauti na hapo hawataishia kukifutia chuo hicho cheti cha ithibati, bali watachukua hatua zaidi za kisheria dhidi ya chuo hicho.
Katika hatua nyingine, kutokana na kuwepo kwa taarifa kuwa zaidi ya wanafunzi 12,000 wamekosa nafasi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2014/15, TCU kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Utawala na Nyaraka, Dk. Savinus Mavoura, imekanusha kuwa hakuna wanafunzi waliokosa nafasi ya vyuo bali wengi walifanya uchaguzi wa vitivo vyenye ushindani mkubwa kwenye chuo kimoja tofauti na mahitaji ya chuo husika.
Alisema hatua hiyo imewalazimu TCU kufanya mchakato wa kutafuta njia mbadala ya kuwapatia nafasi wanafunzi hao katika vyuo vingine kutegemea na chaguo lao, mchakato ambao bado unaendelea kutekelezwa kwasababu nafasi za udahili kwa mwaka huu zimekuwa nyingi tofauti na idadi ya walioomba nafasi hizo.
0 comments: