Thursday, June 12, 2014

Soko la Mchikichi lateketea kwa Moto!

ad300
Advertisement
Eneo la Soko la Mchikichini
TAKRIBAN wafanyabiashara 10,000 wa soko la mitumba la Mchikichini lililoko Ilala Mkoani Dar es Salaam, wamepata hasara baada ya mali zao  kuteketea kwa moto uliounguza soko hilo usiku wa kuamkia jana.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema moto huo ulizuka majira ya saa 4.00 usiku, kwenye vibanda vilivyoko eneo la kusini mwa soko hilo.

Walisema muda mfupi baadae moto ulishika kwenye vibanda vingine na kuanza kusambaa kwa kasi kutokana na uwepo wa bidhaa za nguo zinazopatikana kwa wingi sokoni hapo. 

Jumanne Kangogo ambaye ni Mwenyekiti wa soko hilo, alisema taarifa ya tukio hilo aliipata muda mfupi baada ya kuzuka ambapo alitoka nyumbani na kufika eneo la tukio huku akifanya jitihada za kutoa taarifa kwa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.

Alisema Kikosi hicho kiliwasili eneo la tukio majira ya saa 5 usiku, na kuanza shughuli ya kuzima moto iliyochukua takribani saa 7 mpaka kufikia alfajiri kutokana na ukali na ukubwa wa moto huo.

Kiongozi huyo wa soko alisema hadi sasa hawajajua chanzo cha moto huo wala thamani ya mali zilizoteketea.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo alisema wafanyabiashara wengi wameathirika kutokana na ukweli kuwa hawakua na bima ya aina yoyote, hivyo wamepoteza dira ya maisha yao. 

"Wafanyabiashara wengi hawana tabia ya kukata bima, huo ndio ukweli. Tunaiomba serikali ituangalie kwa namna moja au nyingine kutokana na janga hili lililotupata," alisema Mwenyekiti Jumanne.

Aidha Kiongozi huyo alilishukuru jeshi la Polisi kwa kuweza kulinda mali kadhaa zilizookolewa usiku huo kutoka kwenye moto, baada ya kutokea kundi jingine la watu waliokuwa wakiiba mali hizo.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Ilala aliyeiwakilisha Serikali, Jerry Slaa, alitoa pole kwa wahanga wa tukio hilo na kusema kuwa serikali iko pamoja nao.

Alisema Serikali imeona na imetambua kuwa hasara iliyopatikana ni kubwa, lakini wao kama Serikali wameanza kulishughulikia suala hilo ikiwemo kukutana na Afisa masoko wa Manispaa, Kamati ya uchumi na huduma za jamii ili waweze kupata ufumbuzi.

Sambamba na hilo, alisema Mkuu wa Wilaya Raymond Mushi atafanya vikao na kamati yake ya ulinzi na usalama ili wachunguze na kujua chanzo cha moto huo.

Aidha Meya huyo alisema eneo hilo litabaki kuwa sehemu ya biashara na si vinginevyo, hivyo wafanyabiashara wawe wavumilivu kusubiri matokeo ya upelelezi unaofanywa juu ya tukio hilo.

Wafanyabiashara wakiokoa baadhi ya vifaa.

Meya wa Manispaa Ilala Jerry Slaa (Mwenye miwani), akitoa pole kwa wahanga.


Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: