Advertisement |
Wanahabari chipukizi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika
zoezi la mapambano dhidi ya Rushwa ili hatimaye tatizo hili sugu liweze kupotea
kabisa hapa nchini kwani limeleta matatizo makubwa kama vile kuongeza umasikini
sambamba na kukimbiza wawekezaji kutoka nje.
Wito huo umetolewa na Bibi. Miriam Mseke ambaye ni Afisa wa
TAKUKURU Wilaya ya Kinondoni, wakati akiongea na wanafunzi wa Chuo cha habari
na Utangazaji pamoja na masomo ya ustawi wa jamii cha Royal kilichopo eneo la
Urafiki jijini Dar es salaam wakati alipotembelea chuoni hapo hivi karibuni ili
kutoa elimu kuhusu Rushwa na athari zake kwa jamii ikiwa ni pamoja na kueleza mchango
wa vijana katika suala zima la kupambana na tatizo hili.
Bibi Mseke ameeleza kuwa kwa takwimu zilizopo zinaonyesha
kuwa elimu kuhusu Rushwa bado ni tatizo kwa wananchi walio wengi, jambo
linalosababisha tatizo kushika kasi na kuota mizizi zaidi hapa nchini hivyo wao
kama TAKUKURU wilaya ya Kinondoni wameona wakati umefika sasa kwa wao kutembea
sehemu mbalimbali walipo vijana na kuwapa elimu zaidi kuhusu rushwa sambamba na
kufungua Klabu za mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema Klabu za kupambana na rushwa wamezianzisha ili
kusaidia kuongeza uelewa kwa kundi kubwa la watu kuhusu shughuli zinazo fanywa
na serikali kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na wamelianza sehemu mbalimbali za
wilaya hiyo huku shule na vyuo vikipewa kipaumbele kwani ndipo walipo kundi
kubwa la vijana ambao mara watakapo maliza mafunzo yao wataweza kuwa mabalozi
wazuri sehemu za vijijini kuhusu mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini hivyo
kusaidia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kutokomeza Rushwa.
Mpaka sasa tumeshapita vyuo mbalimbali kikiwemo chuo kikuu cha Dar es salaam pamoja na Chuo cha ustawi wa jamii Kijitonyama, leo tuko hapa Royal tunafahamu mnajua athari za rushwa kwa mtu mmoja na kwa taifa kwa ujumla ikiwemo kushuka kwa pato la taifa, ongezeko la gharama zisizo na ulazima pia kifo hasa kwenye rushwa ya ngono ambayo kwa sasa inatisha sana vyuoni na sehemu mbalimbali za maofisini hivyo tunalileta kwenu suala la klabu tunaomba mtuunge mkono sisi TAKUKURU na serikali yenu kwa ujumla kwani kutokana na fani mnayosomea ni wazi kuwa mtakuwa msaada sana kwa nchi yenu kwenye mapambano haya,” alisema Bi Mseke.
Aidha baada ya kutoa nafasi ya maswali machache kutoka kwa
wanafunzi kuhusu walichokisikia kutoka kwao, Afisa huyo amewataka vijana
kutokata tamaa kwa urahisi katika vita dhidi ya rushwa kwani Serikali iko macho
kwenye mapambano dhidi ya tatizo hilo, hivyo kwa pamoja kwa kushirikiana na
wananchi katika kuwaripoti watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa tatizo
litakwisha kwani wengi wa wanafunzi walilaumu sana TAKUKURU kwa kutofanya kazi
ipasavyo jambo lililo msikitisha Afisa huyo.
Inasikitisha kuona vijana bado hata hamjaingia kwenye soko la ajira lakini mshaanza kuamini kuwa bila rushwa huwezi kupata kazi kwa vigezo vilivyomo kwenye sifa zinazotakiwa na waajiri walio wengi nchini ikiwemo uzoefu kazini usiopungua miaka 2 au zaidi wakati ndo kwanza mtu unatoka chuoni….mnatakiwa kujiamini, na kujipa moyo ili muweze kutetea haki zenu za msingi na sisi kama TAKUKURU tuko nyuma yenu kwa kumpa adhabu stahili mtu yeyote atakaye pindisha kanuni na sheria za ufanyaji wa kazi kama ilivyobainishwa kwenye sheria namba 11 ya mwaka 2007,” alimaliza Bi. Mseke
Muwakilishi huyo kutoka TAKUKURU wilaya ya Kinondoni, alifanikiwa
kufungua klabu ya mapambano dhidi ya rushwa chuoni hapo ambapo jukumu la
kukusanya idadi kamili ya wajumbe na viongozi wa klabu unasimamiwa na mkufunzi
wa chuo hicho Bwana Nsajigwa Mwalugaja ili kuhakikisha zoezi linakamilika.
0 comments: