Tuesday, March 6, 2018

Serikali, WB kukarabati vyuo vikuu nchini

ad300
Advertisement
Serikali imesema baada ya kukarabati miundombinu ya shule kongwe za sekondari nchini, iko kwenye mpango wa kuvigeukia vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

Uamuzi huo imesema umefikiwa kutokana na vyuo vingi vya umma kuwa na miundombinu iliyochoka kwa sababu ya ukongwe wa taasisi hizo muhimu kitaaluma.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, alitoa kauli hiyo jana Machi 5, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizindua kitabu cha 'Facing Forward, Schooling for Learning in Africa' kilichoandaliwa na Benki ya Dunia (WB). 

Alisema mazungumzo ya mradi huo mpya ni kati ya serikali na WB, ambao wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya elimu ambayo kwa miradi yake mitano, inatoa msaada wa fedha takriban Dola za Marekani Milioni 380 (Sawa na zaidi ya Sh. Bilioni 700). 

"WB wametusaidia kwenye miradi mingi, ukiwemo wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) ambao kwa huo serikali imeweza kusimamia ukarabati wa majengo ya madarasa, vyoo na ujenzi mpya hivyo kuwasaidia wanafunzi kwenye upatikanaji wa hali njema, rafiki wa kujisomea," alisema. 

Waziri Ndalichako alisema serikali inaunga mkono hatua zinazofanya na WB, kwenye kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa na mchango kwa maendeleo ya watu na taifa na kwamba mapendekezo yanayotolewa hawayapuuzi. 

Kuhusu kitabu alichokizindua jana, alisema ni kitabu kizuri chenye taarifa nyingi muhimu za kuboresha mazingira ya kujisomea kwa mwanafunzi wa ngazi zote. 

Alisema kuzinduliwa kwa kitabu hicho nchini kwa niaba ya ukanda mzima wa Kusini mwa Sahara, na kuhudhuriwa na Mkurugenzi mwandamizi wa elimu wa WB, Jaime Saavedra, ni heshima kubwa kwa Tanzania.

"Ni heshima kwetu kama nchi kupata bahati ya kuwakilisha ukanda mzima wa nchi za kusini mwa Sahara kwenye uzinduzi huu, hivyo kama ilivyo elezwa kwenye kitabu hiki, nasi tunaamini kuwa shule ni mahali ya kujifunza," alisema. 

Alisema ni wazi kuna wanafunzi ambao wanavuka ngazi moja ya elimu kwenda nyingine huku wakiwa na uelewa mdogo wa waliyoyasoma kwenye ngazi iliyotangulia hivyo upo umuhimu wa ufuatiliaji. 

Kwa upande wake Jaime wa WB alisema kutokana na utafiti wa taasisi yao, dunia ina changamoto ya wanafunzi kusoma, ambayo ina sababisha uchumi kukwama. 

Alisema idadi kubwa ya watu wenye umri wa kwenda shule kwenye nchi za kusini mwa sahara hawajakwenda shuleni hali inayofanya nguvu kazi ya taifa kupotea bila sababu. 

Mkurugenzi huyo wa WB alisema fedha zaidi ni kweli zinahitajika katika mipango ya maendeleo ya sekta ya elimu, lakini mambo makuu matatu ya msingi kwenye maendeleo ya taaluma ni kuwekeza kwenye walimu bora, utawala mzuri wa shule, mitaala na ukaguzi wa shule. 

Uzinduzi wa kitabu hicho chenye nia ya kueleza changamoto za kitaaluma kwenye nchi za kusini mwa jangwa la sahara na namna ya kuzitatua ulishuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Dk. Leonard Akwilapo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa William Anangisye, wanazuoni na wanafunzi kutoka vyuo na shule mbalimbali.

Tanzania inatajwa kuwa ya tatu Afrika kwa kunufaika na fedha za Benki ya Dunia kwenye sekta ya elimu kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali, ambapo wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na ile ya Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zimekuwa zikisimamia miradi husika kimamilifu.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: