Wednesday, March 7, 2018

Korea yatoa vifaa tiba, dawa Mloganzila

ad300
Advertisement
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, amepokea msaada wa dawa na vifaa tiba wenye thamani ya Sh. Milioni 100 kutoka kwa ujumbe wa Kamati za bunge za afya, mazingira na viwanda za Jamhuri ya Watu wa Korea.

Ujumbe huo umekuja nchini kujionea namna Hospitali hiyo ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila, inavyofanya kazi baada ya kuzinduliwa rasmi hivi karibuni.

Kwenye hafla fupi ya makabidhiano hospitalini hapo leo Machi 7, Profesa Ndalichako alishukuru Korea kwa msaada huo na kuwataka wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho kutumia vema miundombinu bora na ya kisasa ya chuo hicho.

"Tumieni vizuri vifaa hivi katika kujifunza ili kujijenga kitaaluma hali itakayomaliza tatizo la uhaba wa wataalamu wa afya nchini," alisema Waziri Ndalichako.

Waziri huyo pia alitumia fursa hiyo kuiomba serikali ya Korea kusini kuendelea kutoa wataalamu wa afya ili kuja nchini kutoa mafunzo ya tiba.

Alisema bado kuna umuhimu mkubwa wa kujengwa hosteli kwa ajili ya wanafunzi na nyumba za walimu katika eneo ilipo hospitali hiyo, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Wakizungumza katika hafla hiyo ya fupi ya makabidhiano mjumbe wa kamati hiyo ya Afya ya Bunge la Korea, Jun Hye Sook alisema msaada huo wa dawa zenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Moja ni ishara ya ushirikiano na udugu mwema.

Alisema Korea itaendelea kutoa ushirikiano katika kuiendeleza Hospitali ya Mafunzo ya Mloganzila kwa msaada wa dawa, vifaa tiba pamoja na wataalamu wa afya.

Mjumbe huyo alisema ana matumaini makubwa kuwa Hospitali hiyo itasaidia kuboresha huduma za afya hasa kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.

Naye Balozi wa Korea hapa nchini Song Geum Young alisema serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuiendeleza Hospitali hiyo kwa kuleta madaktari na wataalamu wa afya.

Akitoa shukrani kwa niaba ya chuo, Kaimu Naibu Kansela wa Huduma za Hospitali wa MUHAS, Dk. Edson Simon alisema msaada unaoendelea kutolewa na Korea utaiwezesha hospitali hiyo kuwa hospitali bora nchini na Afrika kwa ujumla.



Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: