![]() |
Advertisement |

Mafundi
wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakifunga mabomba ya chuma kwa
ajili ya kusimika mfumo wa taa za kuongozea magari katika makutano ya
barabara za Taifa na Pangani jijini Tanga. Mradi huo wa kwanza kufanyika
jijini Tanga unahusiha taa za kuongozea magari na waenda kwa miguu
(traffic lights) katika makutano ya barabara za Taifa na Pangani pamoja
na makutano ya barabara za Swahili, Uhuru na ile ya Hospitali ya Bombo na
utatumia umeme jua.



********************************************
Na Theresia Mwami – TEMESA TANGA
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) inatekeleza miradi miwili ya
taa za kuongozea magari na abiria (traffic lights) jijini Tanga katika
makutano ya barabara za Taifa na Pangani, pamoja na makutano ya barabara
za Swahili, Uhuru na ile inayoelekea hospitali ya Bombo.
Ifahamike kuwa
mji wa Tanga haujawahi kuwa na taa za kuongozea magari na waenda kwa
miguu hapo kabla, zaidi ya kuwa na vipita shoto kwenye baadhi ya
barabara zake.
Akiongea
na Waandishi wa Habari Meneja wa Kikosi cha Umeme TEMESA Mhandisi
Pongeza Semakuwa alisema miradi hii miwili ya taa za barabarani hapa
Tanga inahusisha taa za kuongozea magari pamoja na zile za kuongoza
waenda kwa miguu kuvuka makutano hayo ya barabara.
Taa hizo zitakuwa
zikitumia umeme jua, nishati ambayo itaziwezesha kufanya kazi muda wote
hata pale umeme wa TANESCO unapokuwa na hitilafu.
Naye
Mbunge wa Jimbo la Tanga mjini Mhe. Alhaj Mussa Mbaruku ambae
alipita katika eneo la mradi la makutano ya Barabara ya Pangani na Taifa
maarufu kama “Taifa/Ring Junction” kujionea utekelezaji huo wa mradi wa
Serikali, alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza ajali za
barabarani ambazo zimekuwa zikitokea kwenye makutano ya barabara hizo na
vile vile kuufanya mji wa Tanga kuwa wa kisasa zaidi.
Kwa
upande wake Meneja wa TEMESA Tanga Mhandisi Margareth Gina alisema kuwa
miradi hiyo ya usimikaji wa taa za kuongozea magari na waenda kwa miguu
jijini Tanga imeiingizia TEMESA jumla ya shilingi za kitanzania milioni
434 fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitakazolipwa
kwa TEMESA kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa jiji la Tanga. Aliongeza kuwa
miradi yote miwili iko mbioni kukamilika mapema mwezi huu.
0 comments: