Advertisement |
Elimu ya Awali imetajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya taaluma ya mtoto hasa kwenye ufahamu wake wa kusoma, kuhesabu na kuandika (KKK).
Hiyo imebainika baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Kitengo cha Mawasilino Serikalini, kufanya ziara kwenye baadhi ya mikoa ya kanda ya ziwa na katikati ya nchi.
Ziara hiyo yenye dhamira ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Lipa Kulingana na Matokeo (P4R) na LANES inayoweka msisitizo kwenye KKK, imebaini uhitaji huo baada ya walimu kukiri elimu ya awali ni muarobaini wa mtoto kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Miongoni mwa walimu hao ni Judith Japhet wa shule ya msingi Samia iliyopo Wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza ambaye alisema ufundishaji darasa la kwanza umekuwa rahisi tangu kuanzishwa kwa mradi wa LANES.
"Mradi huu umekuwa na msaada mkubwa kwetu walimu kwa sababu mtoto anakuja darasa la kwanza akiwa tayari anajua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa kiasi fulani," alisema mwalimu huyo.
Aliongeza kuwa hali ya ufundishaji awali kabla ya mradi wa LANES unaowezesha mafunzo ya walimu, usambazaji wa vitabu kuanzia elimu ya awali mpaka darasa la tatu, ulikuwa mgumu kiasi cha mwalimu kukata tamaa na kazi yake.
"Zamani mwalimu ulikuwa unaletewa mtoto darasa la kwanza hata herufi a hajui inavyoandikwa wala kutamkwa, ilikuwa kazi kubwa lakini sasa serikali kupitia mradi huu walimu tunaona faraja na raha ya kazi yetu," alifafanua.
Naye Mwalimu Juliana Segeja, ambaye ni Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Igoma, alisema serikali inastahili pongezi kwa jitihada inazoendelea kuzifanya kwenye uboreshaji wa elimu hasa ya msingi ambayo ndio nguzo ya elimu.
Kwa upande wao Wenyeviti wa Kamati za Shule za Msingi, akiwemo Wilson Lugaka, alisema mradi wa KKK na ule wa lipa kulingana na matokeo umeipa mafanikio makubwa shule yao ya Igoma.
Alisema kutokana na miradi hiyo, kumekuwa na muamko mkubwa wa wazazi na walezi wa wanafunzi kwenye ifuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi kutokana na ukweli kuwa uwezo wa kitaaluma wa wanafunzi husika umekuwa.
"Hapa Igoma mtoto wa darasa kuanzia la kwanza anakusomea vizuri kitabu, anakuhesabia namba na kuandika mwandiko mzuri tu, hili limefanya wazazi kuwa na mwamko chanya kwenye maendeleo ya mtoto wake," alisema.
Wanafunzi kwa nafasi yao waliliambia Uhuru kuwa wanafurahishwa na hatua mbalimbali zinazofanywa na serikali kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na msingi mzuri kitaaluma kwenye nyanja mbalimbali.
Pamoja na pongezi hizo, walitoa rai kuwa kuna umuhimu wa kutolewa waraka kutoka serikalini kwamba mwanafunzi asiyepata elimu ya awali asijiunge na darasa la kwanza ili kumaliza tatizo la wanafunzi wa madarasa ya juu kutokujua kusoma, kuhesabu na kuandika.
0 comments: