Wednesday, August 16, 2017

Utalii wa Kiutamaduni wapewa chapuo

ad300
Advertisement

Katibu tawala wa mkoa wa Kigoma, Charles Pallangyo amewataka wadau wa utalii kuchangamkia fursa za utalii hasa utalii wa kiutamaduni   kwa kuwa ni utalii usiohitaji gharama kubwa katika kuuanzisha.

Amesema watalii wanaokuja nchini kwa sasa wanakuja kwa ajili ya kuijifunza tamaduni zetu kama vile jinsi jamii zetu zinavyoishi na zinavyokula vyakula vyao na si  kuona wanyamapori pekee.

Akizungumza jana mjini Kigoma wakati akifungua  warsha ya kukusanya maoni ya wadau kwa ajili mapitio ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999.  

Palangyo alisema sera hiyo inaboreshwa ili iweze kuendana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani ya kiteknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na mazingira. 

Ukusanyaji maoni huo umeshirikisha wataalamu wa utalii, maofisa utalii, mahotelia, sekta binafsi pamoja na watu wanaojishughlisha na biashara ya utalii moja kwa moja kutoka katika mkoa wa Kigoma, Katavi na Rukwa.

Amesema mikoa ya Magharibi inaweza kujitofautisha na mikoa mingine kwa kuwa na utalii wa kipekee kwa vile ina vivutio vya utalii vya aina mbalimbali ukiachilia mbali Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Mahale na Katavi.

Akitaja baadhi ya vivutio hivyo mbali na hifadhi hizo ni  uwepo wa makabila mbalimbali, nyumba ya makumbusho ya Dkt. David Livingstone, Ziwa Tanganyika, maporomoko ya Kalambo  pamoja na uwepo wa meli ya Mv Liemba.

Awali, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Martini Mrema amesema sera hiyo inapitiwa upya ili kuhakikisha kuwa  utalii  wa nje ya hifadhi  unaanza kupewa kipaumbele tofauti na sasa.
  
Aliongeza kuwa sera hiyo inaboreshwa ili iweze kujibu changamoto za utalii wa sasa 

Kwa upande wake Mdau wa utalii, Jonathan Lucas wa mkoa wa Katavi alichangia kuwa sera hiyo itamke wazi namna mtu mmoja mmoja atakavyonufaika na vivutio vya utalii vilivyopo nchini. 

Mchakato huu wa kukusanya maoni ya wadau unafanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Benki ya Duniani (WB) chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, wadau wa Sekta Binafsi pamoja na  Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT).

Imeandikwa na Lusungu Helela wa Maliasili na Utalii









Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: