Advertisement |
Benki ya Dunia imetoa Dola Milioni 120 ambazo ni sawa na Bilioni 200 za kitanzania kwa ajili ya uwezeshaji wa miradi ya elimu.
Mbali na hiyo pia zitasimamia utoaji wa ujuzi kwa ajili ya kazi zinazoleta uzalishaji wenye tija pamoja na vituo viwili vya umahiri vya kikanda.
Akizungumza katika uzinduzi wa Miradi hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema miradi hiyo itasaidia kuongeza watu wenye ujuzi wa kati ambao watafanya kazi katika sekta za kilimo,Utalii,Ujenzi ,nishati na madini.
Alisema Miradi iliyofadhiliwa ni pamoja na vituo vinne vya umahiri katika masuala ya utafiti wa kilimo na magonjwa ya binadamu,ikiwemo viwili vinavyomilikiwa na Nelson Mandela pamoja na vituo vingine viwili vilivyopo katika Chuo cha Kilimo cha Sokoine University of Agriculture.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania,Malawi ,Burundi na Somalia Bella Bird, alisemaa kuwa uboreshwaji wa rasilimali watu kwa kuongeza ujuzi uliokosekana utasaidia taifa kufikia malengo yake ya kufikia uchumi wa viwanda.
Bella Alisema kuwa inakadiriwa kuwa Vijana milioni 1 huitimu katika vyuo na kuingia katika soko la Ajira kila mwaka hivyo anatarajia kuwa nafasi za ajira kwa vijana hao zitatengenezwa na sekta binafsi iwapo zitashirikiana vyema na serikali .
Kwa upande wake Makamu wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, Karoli Njau alisema kuwa mradi huo utasimamiwa kwa makini ili kuhakikisha kuwa malengo yanafikiwa hususan katika vituo vya umahiri pamoja na mradi wa ujuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye, alisema awali kulikua na upungufu mkubwa wa watu wenye ujuzi nchini hivyo kutokukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Alisema tatizo hilo lililazimu waajiri kuajiri watu kutoka nje jambo linalogharimu fedha nyingi hivyo mradi huo utasaidia vijana 30,000 kupata ujuzi utakaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa kwenye shughuli hiyo ambapo alisema mkoa huo umepata bahati ya kuwa na chuo cha Nelson Mandela hivyo kuwataka wakazi wake kutumia fursa hiyo ipasavyo.
0 comments: