Advertisement |
Serikali ina mpango wa kujenga reli ya kisasa ya Standard Gauge, itakayounganisha kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Lengo
limetajwa kuwa ni ili kuongeza fursa ya kuchagua usafiri sahihi wa
haraka kwa abiria atakayewasili na ndege kupitia terminal II na terminal
III ambayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka ujao.
Kauli
hiyo imetolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, aliyezuru JNIA na kuzungumza na
wafanyabishara wanaofanya shughuli zao kiwanjani hapo wakiwemo madereva
wa taxi.
Alisema tayari
ameanza mazungumzo na wakandarasi kuona namna ambavyo reli hiyo
itajengwa na kukamilika sawa na kukanilika kwa ujenzi wa jengo na
miundombinu ya Terminal III ya kiwanja cha Julius Nyerere.
Waziri
Mbarawa aliyasema hayo akijibu malalamiko ya Mwenyekiti wa madereva
taxi JNIA, kuhusu kunyong'onyeshwa kibiashara na teknolojia ya UBER,
inayofanya shughuli za kubeba abiria kwa bei nafuu zaidi.
Alisema
mbali na usafiri huo unaosambaa kwa kasi nchini hasa kwenye maeneo ya
mijini, teknolojia nyingi zaidi kwenye sekta ya uchukuzi na usafirishaji
wa abiria mengi zitakuja hivyo kuwataka wawe wabunifu kwenye biashara
yao.
Alisema kutokana na
mabadiliko ya sayansi na teknolojia, hakuna sababu ya kulalamika kama
mtu unaendelea kufanya biashara kama zamani kabla ya maendeleo ya
teknolojia, zaidi ya kuamua kubadili biashara iwe ya kisasa.
"Kama
mlivyosikia wakati nyie mnalalamika UBER inawanyima biashara, sisi
serikali tunaleta treni ya kisasa kwenda katikati ya mji hivyo ili
muendelee kuwepo kwenye biashara hii, lazima mbadilike," alisema.
Pia
aliongeza kwa kusema teknolojia inayotumiwa na UBER hapa nchini iko
maeneo mbalimbali kwenye nchi zilizoendelea, hivyo si sahihi kwa
madereva taxi hapa nchini hususan wa JNIA kukaa na kuomba msaada wa
serikali ili kupambana na UBER.
Awali,
Mwenyekiti huyo wa madereva Antipas George, alisema licha ya wao
kufanya kila wanaloagizwa na serikali, biashara yao imekuwa nguvu zaidi
hasa baada ya UBER kuanza kufanya kazi nchini.
"Kwetu
UBER ni tatizo, wakati mimi napanga bei ya kupeleka mteja mjini kwa Sh.
30,000 kutoka hapa Airport, UBER wanamtoza mteja huyo huyo kwa safari
ile ile kwa Sh. 12,000," alilalama.
Baada
ya majibu ya waziri kuhusu hoja yake, madereva hao walishauri serikali
itoe maelezo kwa UBER kutumia taxi ambazo zinalipa kodi zote za serikali
ili kuwe na usawa kwenye biashara hiyo.
Katika
kiwanja cha Julius Nyerere jumla ya taxi 150 mpaka 200 zinaelezwa kutoa
huduma kila siku ambapo kutokana na ujio wa huduma hiyo mpya ya UBER
inayoendeshwa kielektroniki, hali ya kibiashara kwa madereva taxi
imekuwa mbaya.
0 comments: