Monday, August 28, 2017

Hatma ya Urais Kenya, ngoma bado mbichi

ad300
Advertisement
Kesi ya muungano wa NASA kupinga matokeo ya Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta, yaliyotangazwa hivi karibuni na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), imeanza kusikilizwa leo na mahakama kuu ya Kenya.

Mawakili wa kiongozi wa umoja huo wa vyma vya upinzani, Raila Odinga, mapema leo Agosti 28, waliruhusiwa kukagua mitambo ya kielektroniki ya IEBC kama walivyoiomba Mahakama hiyo ya Juu nchini humo.

Hata hivyo, Mahakama iliweka mipaka katika ukaguzi huo uliosimamiwa na msajili wa mahakama hiyo na wataalamu walioteuliwa na majaji ili kulinda usalama wa mitambo husika.

Kwenye ombi waliyowasilisha kwa majaji, mawakili wa Raila walitaka IEBC iamuriwe kuwaruhusu wakague mitambo hiyo wanayohisi ilivurugwa ili kumuongezea kura Rais Kenyatta baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, mwaka huu.

“Tunaelewa kwamba usalama wa mitambo hiyo unapasa kuhakikishwa. Tunaelewa kwamba kuna haki ya kupata habari zinazohifadhiwa na mashirika ya serikali na tunaweka mipaka katika uamuzi wetu,” alisema Jaji Isaac Lenaola ambaye alisoma uamuzi wa mahakama.

Jopo la Majaji liliagiza  msajili wa mahakama kuwasilisha ripoti kabla ya saa kumi na moja jioni leo. 

Wakati wa ukaguzi, NASA iliruhusiwa kuteua wataalamu wawili wa teknolojia ya habari na mawasiliano watakaosaidiana na wataalamu wawili huru walioteuliwa na mahakama na mmoja kutoka idara ya mahakama.

Mahakama pia iliagiza IEBC kuwasilisha ripoti kuhusu idadi ya mitambo ya kutambua wapigakura na kupeperusha matokeo iliyotumiwa (KIEMS), idadi ya mitambo ambayo haikutumiwa na ilipokuwa wakati wa siku ya kupiga kura.

Hata hivyo ilikataa ombi la mawakili wa Raila la kuhusisha kampuni iliyotengeneza vifaa hivyo Safran Morpho kutoka Ufaranza wakisema haliwezi kutekelezeka.

“Kampuni hiyo sio sehemu ya kesi na mahakama haina muda wa kutosha kwa sababu kuihusisha katika kesi hii itachukua muda mrefu,” majaji walisema kwenye uamuzi wao.

Aidha, mahakama ilikubali ombi la NASA la kupatiwa fomu 34a kutoka vituo vyote 40, 883 na 34B kutoka vituo 290 za kujumlisha matokeo katika maeneobunge.

IEBC iliagizwa pia kutoa vifaa vya kukagua fomu hizo pamoja na ripoti mahakamani kabla ya saa kumi moja leo.

Jumamosi ya wiki iliyopita, mawakili wa IEBC na wale wa Rais Kenyatta walitofautiana kuhusu fomu hizo upande mmoja ukisema uko tayari kuziwasilisha kwa NASA endapo mahakama itaagiza hivyo na upande mwingine ukipinga kauli hiyo.

ODINGA AIBUKA MAHAKAMANI

Kiongozi wa NASA na mgombea urais kwa mara nne mfululizo nchini Kenya, Raila Odinga, alifika katika majengo ya Mahakama hiyo saa mbili asubuhi akiandamana na seneta mteule wa Bungoma Moses Wetang’ula na kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi.

Mara baada ya kuonekana na wafuasi wake, kulikuwa na vurugu kwa dakika kadhaa baada ya Raila kukutana uso kwa uso na maofisa wa usalama waliowazuia baadhi ya watu aliofuatana nao kuingia mahakamani. 

Hali kama hiyo ilimpata mgombea mwenza wake, Stephen Kalonzo Musyoka, ambaye pia alifika baada ya dakika chache na maofisa wa usalama walikataa kuwaruhusu watu alioambatana nao.
 
Kabla ya kuanza kuwasilisha kesi, wakili wa Raila James Orengo, aliwatambua vinara wa NASA na viongozi wachache wa Jubilee waliokuwemo mahakamani humo.

“Ninataka kufahamisha korti kwamba walalamishi wako kortini. Viongozi wa ule upande mwingine pia wako hapa na ninafikiri hii ni hatua nzuri,” alisema Orengo.


Usalama uliendelea kudumishwa ndani na  nje majengo ya Mahakama ya Juu huku baadhi ya barabara zikifungwa.

Maofisa wa polisi waliendelea na doria katika barabara zote zinazokwenda kwenye jengo hilo la mahakama, ambazo kamanda wa polisi jijini Nairobi, Japheth Koome aliviambia vyombo vya habari zitafungwa hadi Ijumaa kesi itakapoamuliwa.

TUME YASISITIZA UCHAGUZI ULIKUWA HURU NA HAKI 100%

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumatatu ilisisitiza kuwa iliandaa uchaguzi huru na wa haki ambao Rais Uhuru Kenyatta alishinda.
Wakili wa tume hiyo, Paul Muite, alisema mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati hakukosea kumtangaza Rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8 na kuwataka majaji wa Mahakama hiyo kufuata sheria katika kuamua kesi ya kupinga matokeo ya kura ya urais.

“Wakenya walizungumza kupitia kura na mapenzi yao hayawezi kukosolewa. Uchaguzi uliandaliwa kwa njia huru kulingana na sheria na matokeo yalikuwa halali,” alisema Muite.

Aliendelea kufafanua kwamba, mawakili wa NASA hawakuthibitisha kwamba kulikuwa na dosari katika vituo vya kupigiakura.

“Ni katika vituo ambapo kura za urais hutangazwa na kupeperushwa hadi kituo cha kujumlisha matokeo katika maeneobunge,” alisema.

Wakili Paul Nyamodi aliambia mahakama kwamba fomu zote vituoni hutiwa saini na mawakala wa wagombeaji mbalimbali.

Alisema matokeo yalioonyeshwa katika kituo cha kujumlisha matokeo cha Bomas of Kenya yalikuwa ya muda tu na tume ilifanya hivyo kutimiza uamuzi wa korti.

Kwa upande wao, Mawakili wa NASA wakati kesi ikiendelea walifichua jinsi mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati alivyomtangaza Rais Uhuru Kenyatta mshindi kabla ya kupokea matokeo ya vituo vyote 292 vya kujumlisha kura. 

Katika malalamiko yao, mawakili James Orengo na Otiende Amolo walidai Chebukati alimtangaza Rais Kenyatta mshindi siku nne kabla ya kupokea matokeo kutoka maeneo yote kinyume cha sheria za uchaguzi.

Alisema hiyo ni sehemu tu na kwamba uozo zaidi utaanikwa baada ya mitambo ya kupokea na kupeperusha matokeo kufunguliwa kubaini jinsi kura kutoka vituo visivyo rasmi zaidi ya 10,000 vilivyotumwa katika kituo cha kitaifa cha kujumulisha matokeo ya kura za urais (NTC) cha Bomas jijini Nairobi.

Wakati huo huo, mawakili hao walidai kwamba mpaka sasa Chebukati bado hajatangaza idadi ya kura zilizoharibika za kila mgombea urais kati ya wote nane wa kiti cha urais kama inavyotakiwa kisheria.

"Chebukati alisema Agosti 11, mwaka huu kura zilizokataliwa na kuharibika ni 477,000 kisha akasema mnamo Agosti 18 kura zilizoharibika ni 403,003 na mwishowe akasema kura zilizoharika ni 81,685.

“Je, kura zilizoharibika ni ngapi hasa na Chebukati alimtangaza Rais Kenyatta mshindi mnamo Agosti 11 ilhali katika barua aliyoandikia viongozi wa NASA, Agosti 14 alikiri alikuwa hajapokea matokeo kutoka maeneo yote,?" alihoji.

Aliongeza kushangaa kuwa kama IEBC haikuwa na ushahidi wa Fomu 34A na 34B kuthibitisha Kenyatta alishinda kwa njia inayofaa, Chebukati aliwezaje kujua mshindi kabla ya kupokea matokeo kutoka maeneo 187 ya uwakilishi bungeni.

Pamoja na hayo, aliongeza kuwa kufikia Agosti 11, Chebukati alikuwa amepokea Fomu 34A 29,000 kutoka kwa maafisa wa IEBC ikiwa ni nusu ya Fomu zaidi ya 40,883.

Matokeo feki

“Ukaguzi wa hati zaidi ya 54,000 zilizowasilishwa na IEBC umebaini matokeo feki yalitangazwa na IEBC kutoka maeneo yasiyojulikana,” alisema wakili huyo.

Jaji Mkuu (CJ) David Maraga, naibu wake (DCJ) Philomena Mwilu, Majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaac Lenaola walielezwa kwamba kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria za uchaguzi, ufisadi na ushawishi kutoka kwa Rais Kenyatta.

“Kutokana na uigizwaji wa kura katika mitambo ya IEBC utaratibu fulani ulidumishwa uliomweka Rais Kenyatta mbele kwa asilimia 54 na Odinga 44,” alisema Amolo.

Wakili huyo alisema matokeo ya kwanza ya kura za urais hayangekuwa tayari kwa vile yalianza kutangazwa saa 11 na dakika saba na “bado ROs walikuwa wanaendelea kuyapokea kutoka vituoni. Je, matokeo haya yalipigwa kutoka maeneo gani ya uwakilishi?”

Kura milioni 7

Majaji hao walifahamishwa  kuwa kura zaidi ya milioni 7 kutoka vituo visivyo rasmi vya kupigia kura zilitumwa katika kituo cha kitaifa cha kujumulisha kura (NTC) kutoka vituo 10,480.

Pia mahakama ilifahamishwa na utetezi wa NASA kuwa kura za Odinga ziliibwa na maofisa wa IEBC na kujumulishwa katika kura za Rais Kenyatta na maofisa wa IEBC.

“Matokeo ya uchaguzi wa urais yaliborongwa kwa viwango vya juu kumfaidi Rais Kenyatta,” walisema mawakili Orengo na Amolo

Orengo alienda mbali zaidi na kuwaambia majaji hao kwamba ushahidi uliowasilishwa na IEBC kortini ni tofauti na ule waliopewa na kwamba kulikuwa na ukiukaji usio na kifani wa sheria za uchaguzi hasa Kifungu 134(a)(ii) kuhusu upokeaji, ujumlishaji na urushwaji wa matokeo ya kura za urais kuanzia vituo vya kupigia kura hadi utumaji kwa njia ya kiteknolojia matokeo hayo na msimamizi wa uchaguzi katika kila eneobunge.

Sheria kukiukwa

“Uchaguzi mkuu uliopita ulikuwa unaendeshwa kwa njia ya kiteknolojia na kwamba maofisa wa IEBC walitakiwa kupiga picha Fomu 34A na Fomu 34B kabla ya kutuma kwa NTC Bomas,” alisema Orengo kuongeza, “hili halikufuatwa kwenye uchaguzi huu.”

Alisema maagizo ya majaji watano wa mahakama ya rufani kwa IEBC yalikuwa maofisa waliosimamia uchaguzi katika maeneo 290 (ROs) watangaze moja kwa moja matokeo ya urais na kuyarusha kwa kituo cha NTC yajumulishwe kisha mshindi atangazwe, lakini hawakufanya hivyo.

Mawakili hao walikamilisha hoja zao huku wakiwaomba majaji hao saba wafutilie mbali  ushindi wa Rais Kenyatta kwa vile walichokiita hakuchaguliwa na sheria za uchaguzi na katiba ya nchi hiyo.

Stay tuned kesho panapo majaliwa kujua yanayoendelea...
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: