Advertisement |
Wapenzi wa soka wilayani Lushoto mkoani Tanga wameeleza
kusononeshwa na matokeo ya awali ya timu zao mbili zinazowakilisha makao makuu
ya wilaya kwenye ligi ya mkoa inayosimamiwa na Chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tanga (TRFA).
Timu hizo ni Lushoto Star pamoja na Lushoto shooting ambazo
zote mbili zilicheza mchezo wao wa kwanza tarehe kumi ya mwezi huu kwenye
viwanja viwili tofauti.
Lushoto Star walikuwa uwanja wa nyumbani (Hazina) wakiwakaribisha
Eagle Rangers ya Tanga mjini na kuambulia kipigo cha 3-1 kwenye dakika 90 zilizokuwa
za piga ni kupige kila timu ikitaka kuwaridhisha wapenzi wa soka waliohudhuria
mtanange huo kwa kuonyesha kandanda safi lakini mwisho wa siku waswahili
walisema ‘mpira magoli’, wageni waliondoka na ushindi huo mnono.
Huko Muheza nako, Timu ya halmashauri ya Muheza iliwakaribisha
wawakilishi wengine wa wilaya ya Lushoto, timu ya Lushoto Shooting na bila
hiyana wakawachabanga bao 3-0 na kujihakikishia nafasi nzuri mara watakapo
rudiana kwenye mzunguko wa pili wa ligi kwenye mechi itakayochezwa mjini Lushoto.
Matokeo hayo yamechukuliwa kwa mtizamo tofauti na wadau wa
soka wilayani hapa, kwani walitegemea matokeo mazuri zaidi toka kwa timu zote
mbili kutokana na jinsi wanavyozijua timu hizo na mpira wanaoucheza.
Akiongea na willyshechambo blog mmoja wa wadau
hao Bw. Pius Kinyashi amesema:
Lushoto bado ina safari ndefu sana kutoka kwenye kandanda, yaani wenzetu huwa hawafanyi kosa kwenye mechi za ufunguzi kabisa. Sasa kwa jinsi matokeo yalivyo kwa timu zote mbili, hali ni ngumu sana mzunguko wa pili, japokuwa mpira hautabiriki lakini bwana mi nazijua hizi timu za Tanga mjini wana defence sana wakijua walishinda round ya kwanza ili wapate hata sare ya bila kufungana.
Aidha mchezaji wa Lushoto Star anayechezea nafasi ya kiungo
John Godfrey amesema wamejifunza kutokana na makosa, wamekubaliana na matokeo wanaangalia
mechi zijazo.
Tumefungwa tena nyumbani ni aibu hasa kwa mechi ya kwanza, ila Coach katuelekeza wapi tumekosea hivyo tunamuomba tu Mungu game zijazo tufanye poa, ni hayo tu.
0 comments: